Mwenyekiti CCM Dodoma kizimbani tuhuma rushwa

26Mar 2020
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Mwenyekiti CCM Dodoma kizimbani tuhuma rushwa

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Mjini, Robert Mwinje (39), amefikishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma, akikabiliwa na mashtaka ya kula njama, kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo za uteuzi wa waombaji wa uongozi ndani ya chama hicho.

Mwinje aliondolewa katika nafasi yake Desemba 18 mwaka jana kutokana na kile kilichoelezwa na chama kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, alisema kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wamemfikisha Mwinje na Nyemo Malenda (20) kwa makosa hayo.

Kamanda Kibwengo alisema Mwinje na mwenzake wanadaiwa kutenda makosa hayo kinyume cha Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 na marejeo ya mwaka 2018.

“Uchunguzi wetu umeonyesha kwamba kati ya tarehe 18 na 20 Oktoba 2019, Mwinje na Malenda ambaye ni Mhudumu wa Ofisi, walighushi barua ya uteuzi wa waomba uongozi ndani ya chama na huku wakijifanya imetolewa na uongozi wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, wakaikabidhi kwa mwanachama mmoja kwa hatua huku wakifahamu kwamba ni uongo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Takukuru imempandisha kizimbani Mwalimu Mkuu wa Shule Msingi Msisi ya Wilayani Dodoma, David Mdeka (44), kwa tuhuma za matumizi mabaya ya nyaraka na kumdanganya mwajiri kwa kughushi muhtasari wa kikao na kutoa benki Sh. milioni moja.

Alisema mwalimu anadaiwa kutoa fedha hizo benki na kuzifuja kwa maelezo ya kununua vifaa ambavyo havikufikishwa shuleni na ukarabati haukufanyika.

Pia, Kibwengo alisema wanatarajia kumfikisha mahakamani Ofisa Mtendaji wa Kata ya Thawi wilayani Kondoa, Hashimu Ally (42), kwa madai ya kuomba rushwa ya Sh. 155,000, akidai kuwa tayari alishapokea Sh. 60,000 kutoka kwa mwananchi ili asimchukulie hatua kwa kosa la mjukuu wake kutohudhuria shuleni kwa siku 31.

Alidai kuwa baada ya kufanyika uchunguzi, ilionyesha mwanafunzi huyo alifuata taratibu za uhamisho na kufanikiwa kwenda shule nyingine.

Pia, Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Wilaya ya Bahi, Adam Richard (49), amefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka manne ya kuomba rushwa ya jumla ya Sh. milioni 3.5 huku akidaiwa kupokea Sh. 1,050,000 kutoka kwa walimu wanne ili awasaidie katika mchakato wa kupandishwa madaraja.

Aliwataka watumishi wa umma kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za utumishi na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Habari Kubwa