Mwenyekiti Mahakamani kuomba,kupokea rushwa

06Apr 2020
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
Mwenyekiti Mahakamani kuomba,kupokea rushwa

TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa ( TAKUKURU) mkoani Katavi inatarajia kumfikisha mahakamani Mwenyekiti wa Kijiji cha  Igagala wilayani Tanganyika mkoani humo kwa tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa ya kiasi cha sh 80,000.

Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi John Hunja

Akizungumza na waandishi Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi, John Hunja amesema kuwa mtuhumiwa Lawrence Shilla (56) ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji cha Igagala ameomba na kupokea rushwa kutoka kwa mfanyabiashara wa vyuma chakavu.

Hunja amesema mtuhumiwa hiyo alitenda kosa hilo march 27 mwaka huu ambapo ni kinyume na kifungu cha 15 (1) (a) na (b) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

" Hii leo tunatarajia kumfikisha mahakamani Lawrence Danford Shilla huyu ni mwenyekiti wa kijiji cha igagala kwa tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa ya kiasi cha Shilingi 80.000 kutoka kwa mfanyabiashara wa vyuma chakavu ," amesema Hunja.

Aidha, Hunja amesema mtuhumiwa  huyo alituma askari wa Jeshi la akiba (mgambo) kumkamata na kumfikisha ofisini kwake mfanya biashara huyo na kumueleza anatakiwa kulipa ushuru wa kiasi hicho cha pesa ili aruhusiwe kufanya biashara katika Kijiji hicho.

Hunja amesema mtuhumiwa huyo alishikilia baiskeli, kitambulisho na vyuma ambavyo mtoa taarifa alikuwa tayari amekwisha vinunua.

Takukuru Wilaya ya tanganyika iliandaa mtego na kufanikiwa kumkamata majira ya saa 3 usiku katika ofisi za serikali ya kijiji hicho, hata hivyo Takukuru inatoa wito kwa watumishi wa umma na jamii kwa ujumla kutojihusisha na vitendo vya kijinai kama kuomba na kupokea rushwa.

Habari Kubwa