Mwili wa Magufuli wazungushwa mara tano kuridhisha Wananchi

21Mar 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mwili wa Magufuli wazungushwa mara tano kuridhisha Wananchi

MARA baada ya shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli kusitishwa katika Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam kutokana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe alitangaza utaratibu wa kuaga mwili kwa kuuzungusha uwanjani hapo.

Baada ya kutangazwa kwa utaratibu huo Mwili huo ulipakiwa kwenye gari maalum lililokuwa na maofisa wa Jeshi na kuzungushwa katika uwanja huo mara tano ikiwa ni baada ya maelfu ya wananchi kuulizwa wanataka uzungushwe mara ngapi.

“Wananchi mwili utazunguka uwanja ukiwa kwenye gari mara tatu, kila mmoja pale alipo apunge mkono, tufanye kama bungeni wanaokubali  mara tatu waseme ndiyo,” amesema Gondwe lakini wananchi walikaa kimya.

Ndipo Mkuu huyo wa Wilaya akauliza tena, “wanaosema hapana,” na wananchi wakajibu, “HAPANA” lakini aliposema mwili wa kiongozi huyo uzungushwe mara tano ili wamuage wananchi hao waliitikia kwa sauti, “NDIO.”

Kuanzia saa 9:23 alasiri gari lenye mwili huo lilianza kuzunguka uwanja huo huku mamia ya wananchi wakipunga mkono na wengi kuonekana wakifuta machozi. Msafara ulizunguka uwanja huo hadi saa 10:10 jioni na kuanza safari ya kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa ajili ya safari ya Dodoma.

Habari Kubwa