Mwili wa Prof. Baregu kuagwa leo 

17Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mwili wa Prof. Baregu kuagwa leo 

MWILI wa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mwanazuoni nguli, Prof. Mwesiga Baregu, unatarajiwa kuagawa nyumbani kwake leo, Kunduchi, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii na Katibu Mkuu wa CHADEMA, kiongozi na mwanazuoni huyo ataagwa kabla ya kusafirishwa kwenda mkoani Bukoba mkoani Kagera kwa maziko.

“Juni 17, mwaka huu, mwili utaletwa nyumbani Kunduchi, Juni 18 ibada na kuaga kanisani Kunduchi, Juni 19 kusafirishwa na Juni 20 mazishi Bukoba Vijijini (Maruku/Batairuka,” ilibainisha taarifa hiyo.

Mwanazuoni na mwanasiasa huyo aklifariki dunia Juni 13, mwaka huu, baada ya kukaa chumba cha uangalizi maalum kwa siku 15 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

 Prof. Baregu atakumbukwa kama msomi aliyefanya siasa bila kuharibu kazi zake za kitaaluma na Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba.

Alikuwa profesa wa sayansi ya siasa na utawala wa umma na profesa nguli wa masuala ya uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hadi mwaka 1998 alipostaafu kwa mujibu wa sheria.

Baada ya hapo alifanya kazi kwa mkataba hadi mwanzoni mwa miaka ya 2010 alipositishiwa mkataba wake kwa kile kilichoelezwa kuchanganya utumishi na siasa. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT).

Mbali na kuwa mwanataaluma, Prof. Baregu alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA hadi mwaka 2019.

Habari Kubwa