Mwinyi ahakikishia diaspora ushirikiano

19Oct 2020
Rahma Suleiman
Dar es Salaam
Nipashe
Mwinyi ahakikishia diaspora ushirikiano

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema wanaoishi nje ya nchi (Diaspora), wana mchango mkubwa wa kusaidia uchumi wa nchi kwa kuwekeza nchini ili Taznania ikiwamo Zanzibar kupata maendeleo.

Aliyasema hayo Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi ikiwa ni muendelezo wa kampeni zake na kukutana na makundi ya watu mbalimbali.

Alisema endapo atapata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar, anakusudia kufanya mapinduzi katika kukuza uchumi kwa kushirikiana na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Alisema iwapo ataingia madarakani, atahakikisha anaweka mazingira mazuri kwa diaspora kuona wanaendelea kusaidia maendeleo ya nchi yao.

Dk. Mwinyi, aliwapongeza kwa utayari wao katika kuwasaidia Wazanzibari wenzao ambayo ndio azma ya serikali kushirikisha watu mbalimbali waliopo katika nchi mbalimbali kusaidia nchi yao.

"Azma yetu ya Chama Cha Mapinduzi katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi, kundi lenu tunalihitaji sana katika hili ikiwamo kupata wataalamu wazalendo ambao mtasaidia kukuza uchumi wetu kupitia sekta mbalimbali hasa uchumi wa bahari kuu," alisema.

Dk. Mwinyi aliwahakikishia Wazanzibari nje ya nchi ambao wapo tayari kurudi nyumbani, Serikali ipo tayari kuwatumia katika utaalamu wao katika sekta mbalimbali.

Hata hivyo, alisema anatambua juhudi zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya saba kwa kutengeneza sera na sheria ya diaspora, na kuahidi atakapoingia madarakani ataaza kutekelezwa mara moja.

Aliahidi kulinda maslahi ya diaspora kwa kile wanachokiwekeza na kupata haki zao kama wazawa.

Aliwaomba kuendelea kutoa misaada katika nchi yao na kufikiria kufanya makubwa zaidi hasa kuimarisha huduma mbalimbali za kitaalamu.

"Tunataka kuwa na hospitali ya rufani ambayo itakuwa na wataalamu mbalimbali, hatutaki kuona mgonjwa wa moyo anapelekwa sehemu nyingine, lengo letu atibiwe hapa hapa kama wanavyofanya wenzetu Tanzania bara kwa Hospitali ya Jakaya Kikwete," alieleza.

Alisema katika kufanikisha hilo, ni jukumu la serikali kuona inaweka mazingira mazuri ikiwamo vifaa tiba na mambo mengine muhimu.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya ushirikiano na uratibu wa Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi, Adila Hilal Vuai, alisema lengo la diaspora ni kushirikiana katika maendeleo ya nchi yao ikiwa ni dhamira ya serikali ya awamu ya saba chini ya Dk. Ali Mohamed Shein.

Alisema, wapo Wazanzibari wanaoishi nchi mbalimbali zikiwamo Denmamk, Oman, Uk, Jaman, Ethiopia, China, Canada na nchi nyengine, ambao ni wachangiaji wakubwa katika nchi yao kupitia sekta mbalimbali zikiwemo elimu na afya.

Kwa upande wao, Diaspora walisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kutokubalika kumiliki ardhi kwa kisingizio sio wazawa na kutotambulika na masheha katika maeneo wanayoishi wakiwa Zanzibar.

Habari Kubwa