Mwinyi akiri ulikuwa mtihani mgumu

11Jul 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mwinyi akiri ulikuwa mtihani mgumu

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Licha ya kuibuka kidedea, mgombea huyo amekiri kuwa mchuano huo tangu kuanza mchakato wa kuchukua fomu, haukuwa kazi rahisi kwake ndiyo maana hata mwili umepungua.

Dk. Mwinyi aliibuka mshindi katika kura zilizopigwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kwa kupata kura 129 sawa na asilimia 78.65 ya kura zote.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema Dk. Mwinyi aliwashinda Dk. Khalid Salum aliyepata kura 19 (asilimia 11.58 na Shamsi) Vuai Nahodha, kura 16 sawa na asilimia 9.75 ya kura zilizopigwa,

Baada ya Ndugai kutangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli alisema kwa matokeo hayo wajumbe wameamua kwa hiari yao bila kulazimishwa wala kushurutishwa na mtu.

“Kwa upendo wenu ninyi wenyewe moyoni, kwa kumtanguliza Mungu wenu, kwa ajili ya ushindi mkubwa wa CCM Zanzibar na kwamba aliyechaguliwa mtakwenda kumtetea kwa nguvu zenu zote kwa ajili ya ushindi wa CCM na kwa masilahi mapana ya CCM. Dk. Hussein Mwinyi ndiye atakuwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar,”alisema.

“Dk. Mwinyi aliyeongoza kwa kupata kura asilimia 78.65 katika kura zote zilizopigwa hapa bila kuharibika hata kura moja ndiye aliyeteuliwa na kikao hiki cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi katika kinyang’anyiro cha urais wa Zanzibar,” alisisitiza.

ILIKUWA KAZI NGUMU

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Dk.Mwinyi alisema ilikuwa kazi ngumu tangu kuanza kwa kinyang’anyiro hicho ndani ya CCM.

“Zoezi hili halikuwa rahisi. Katika maisha yangu nimefanya mitihani mingi lakini mkubwa kuliko yote ulikuwa huu. Ukiniona nimepungua sababu ni hili. Najua kazi iliyo mbele yangu ni kubwa lakini haitakuwa yangu peke yangu nitakuwa na ninyi.

"Ni kweli tulikuwa 32, kamati maalumu tulipatikana watano mimi nikiwemo. Nashukuru sana kwa hatua ile lakini baada ya pale, Kamati Kuu jana imeweza kutoa wagombea watatu na hatimaye leo nimepatikana mimi kama mgombea au mpeperusha bendera ya CCM katika nafasi ya urais Zanzibar. Hii ni heshima kubwa sana na kura nilizopata 129 ni nyingi sana. Hii inaonesha imani yenu juu yangu na mimi ninataka niwaahidi kwamba nitafanya kazi. Nitalitumika taifa hili kwa uwezo wangu wote," alisema.

"Kinachonipa faraja ni kwamba pamoja na kwamba tulikuwa 32 na hatimaye niko mimi wenzangu wote wako tayari kushirikiana nami,"

Awali, akiomba kura, Dk. Mwinyi aliahidi endapo atachaguliwa, ataenzi Mapinduzi ya Zanzibar na kudumisha Muungano na kuyaendeleza yale yote mazuri yaliyofanywa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

“Vilevile niwaahidi nitatekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM mwaka 2020 hadi 2025 itakayotolewa kwa upande wa Zanzibar. Kwa heshima na taadhima na kwa unyenyekevu mkubwa naomba mnipigie kura nyingi za ndiyo mimi Hussein Ali Mwinyi,” alisema.

JMP NA MBELEKO

Kabla ya kuanza kupigwa kura na baada ya wagombea watatu kumaliza kujieleza, Rais John Magufuli alimtaka Dk. Shein kutoa neno kwa kuwa katika kampeni mtu anaweza kusema ametumwa na fulani.

“Mtu anaweza kusema nimetumwa na huyu, huyo chaguo la fulani. Mimi walikuwa wanasema chaguo langu ni (Prof. Makame) Mbarawa nimemleta nimembeba. Sasa sifahamu leo watazungumza nani. Kura zitapigwa humu na kuhesabiwa hapa hapa,” alisema.

Aliwaambia wajumbe kwamba kinachohitajika ni ushindi katika uchaguzi mkuu na si kwenda kujaribu kushinda, hivyo kuwataka kumchagua mtu atakayekwenda kushinda. Alisema katika dhamira zao kila mmoja ajitafakari atakayemchagua na ushindi lazima upatikane.

Kauli ya Prof.Mbarawa

Akizungumza miongoni mwa wagombea walioingia katika majina matano, Prof.Makame Mbarawa alishukuru chama kwa kumpa heshima ya kuwa miongoni mwa waliochukua fomu huku akisema safari hiyo haikuwa rahisi.

“Tulikuwa wengi, tulipita kwenye milima na mabonde mengi, maneno mengi mazuri na mabaya lakini leo jahazi yetu imefika bandarini na lengo letu ni moja tu CCM kupata ushindi,”alisema.

Aliongeza “Naomba nikuhakikishie Mwenyekiti yule ambaye leo hii atakuwa mshindi huyo ndo atakuwa mshindi wetu na Rais Zanzibar, mimi saa zote wakati wote nitatoa muda wangu kumhudumia yeye ili kupata ushindi.”

Dk. Shein, ambaye ameongoza Zanzibar kwa miaka 10 na anamaliza muda wake, aliposimama alisema hajambeba mtu yeyote kati ya wanachama waliojitokeza kutaka kumrithi.

“Mimi sijawa na mgombea na sitakuwa na mgombea. Sijambeba mgombea, sijapata kufanya hivyo. Kila mwanachama ana haki ya kugombea CCM. Yasitangazwe ambayo hayapo, najua yamesemwa kwamba Hamisi Mussa chaguo la Rais na jana tumesikia Rais kasemwa anambeba Mbarawa, na mimi sijambeba Mussa, muulizeni na wala sitafanya hivyo,” alisema Dk. Shein.

Alisema ameyasema hayo waziwazi kwa kuwa wengine hupenda kuhusisha kuwa viongozi wa juu wana watu mtu wao wamemweka mfukoni watamtoa.

“Kwa mimi mfuko wangu wa shati haingii Bwana Hamis Mussa. Watafute mengine waseme waliyotaka kusema wasiseme hili. Ana haki yake na chama hiki, kachukua fomu kajaza, kapita alikopita Kamati Kuu haikumpitisha. Tusihusishwe sisi bure, mimi sijawahi kuhusishwa tangu niwe kwenye chama, hebu tuwe waungwana. Tuseme yale tunayotakiwa kusema,” alisema.

Habari Kubwa