Mwinyi akunwa utendaji Magufuli

24Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mwinyi akunwa utendaji Magufuli

RAIS wa pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi amesema amevutiwa na kasi ya Rais John Magufuli katika kupiga vita rushwa na kumpongeza kwa kazi hiyo, imeelezwa.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais iliyotolewa jana ilisema Alhaji Mwinyi alitoa pongezi hizo baada ya kukutana na Magufuli Ikulu, jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu ilisema Rais mstaafu Mwinyi alifika na kufanya mazungumzo na Magufuli kwa mara ya kwanza, kwa lengo la "kumpongeza kwa kutimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani na pia kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake."

Alhaji Mwinyi, taarifa hiyo ilisema, alitaja baadhi ya maeneo ambayo Rais Magufuli amepata mafanikio makubwa kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa.

Taarifa ilisema mzee Mwinyi anaona hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Magufuli zimedhihirisha kasi kubwa ya kukabiliana na tatizo la rushwa ikilinganishwa na wakati uliopita.

"Rushwa ilikuwepo tangu enzi ya (Rais wa kwanza) Hayati Mwalimu Nyerere, aliipondaponda kabisa lakini hakuimaliza," taarifa hiyo ilimnukuu Alhaji Mwinyi.

"Na sote tuliosalia ni hivyo hivyo, kila mmoja amefanya kwa kiasi chake, lakini Rais Magufuli kwa mwaka mmoja ameleta sunami, nafurahi sana."

Eneo jingine ambalo utendaji wa Rais Magufuli umemkuna mzee Mwinyi, kwa mujibu wa taarifa, ni kuimarishwa kwa utendaji kazi Serikalini.

Alhaji Mwinyi amekaririwa akisema hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Rais Magufuli zimeongeza kasi zaidi na kwamba ametoa wito kwa viongozi na wananchi kuunga mkono juhudi hizo.

"Tuliobaki tumsaidie, tumsaidie kwa kumuombea dua," taarifa imemkariri.

"Tumsaidie kurekebisha kwa kusema ukweli pale ambapo watu wanapotosha, tuseme sio hivyo, ilivyo ni kadhaa kadhaa kadhaa.
"Tusiwaache watu wakapata nafasi ya kuongea uongo, kila mtu anaweza kuwa anasema kutokana na nia yake na lengo lake, lakini hakuna asiyejua kuwa kazi aliyoifanya mwenzetu ni nzuri nzuri nzuri ya ajabu."

Wakati huo huo, taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema kiongozi huyo jana alikutana na kufanya mazungumzo ofisini kwake Magogoni na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Habari Kubwa