Mwinyi amtembelea Lissu hospitalini

06Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mwinyi amtembelea Lissu hospitalini

Wiki moja tangu Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amtembelee Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, katika Hospitali ya Nairobi, Kenya, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, naye alifika hapo jana kumjulia hali mgonjwa huyo.

Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi akiwa hospitali ya Nairobi Kenya kumjulia hali Mwanashera wa Chadema, Tundu Lissu

Samia amtembelea Lissu baada ya kumalizika kwa hafla ya kumwapisha Rais Uhuru Kenyatta kuongoza Kenya kwa muhula wa pili katika uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi Novemba 28.

Makamu wa Rais alimwakilisha Rais John Magufuli katika sherehe na ziara hiyo wodini kwa Lissu.

Lissu alipelekwa katika hospitali hiyo baada ya Chadema kuona anahitaji huduma zaidi kuliko alizopata katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma Septemba 7, baada ya kushambuliwa kwa risasi 32 na watu wasiojulikana mchana huo.

Kati ya risasi hizo alizorushiwa nje ya nyumba yake katika eneo la Area D, mjini Dodoma, wakati akitoka katika kikao cha Bunge, tano zilimpata maneo mbalimbali ya mwili na amefanyiwa operesheni 17 Dodoma na Nairobi tangu hapo.

Akizungumza juzi na Nipashe katika mahojiano maalum, IGP Sirro alisema wametuma wapelelezi Nairobi baada ya kusikia Lissu amekubali kuhojiwa juu ya tukio hilo na matarajio yao pia ni kuwapata dereva na mlinzi wake.

“Tumetuma watu wetu kwenda kuchukua maelezo yake (Lissu)," alisema IGP Sirro. "Mwanzo tuliomba kwenda lakini chama (Chadema) walikataa. Juzi tumesikia wamesema wako tayari".

"Tumetuma vijana wetu wawili kwenda Nairobi kuchukua maelezo yake.”

Alisema lengo kubwa ni kujua mazingira ya shambulio yalikuwaje na kwamba ikiwezekana wampate dereva na msaidizi huyo wa Lissu ili kurahisisha upepelezi wa tukio lenyewe.

“Upelelezi unaingia vitu vingi sana (sasa) kutompata dereva na mlinzi wake Lissu inashindwa kutupa picha kamili ya tukio,” alibainisha.

“Niwaambie Watanzania watuamini, hatuko kwa ajili ya kuona hatumtendei mtu haki, tupo kwa ajili ya kutenda haki.”Mara baada ya Lissu kupigwa risasi, Bakari alikuwa mmoja wa watu waliompeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kisha kupanda naye ndege iliyompeleka Nairobi usiku huo kwa matibabu zaidi. 

Habari Kubwa