Mwinyi asisitiza kudumisha Muungano

16Oct 2021
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Mwinyi asisitiza kudumisha Muungano

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha Muungano kwa kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kufanya biashara bila bughudha yoyote.

Dk. Mwinyi alisema hayo wakati akizindua miradi minne ya Jeshi la Magereza iliyoko mkoani hapa.

Akizindua miradi hiyo, Dk. Mwinyi alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpa nafasi ya kufanya kazi hiyo ambayo ni kwa miradi ya Ngome ya Gereza la Mkono wa Mara, jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto, nyumba za makazi ya maofisa na askari pamoja na kiwanda cha maziwa cha Kingolwira kwa niaba yake.

Pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kuwaletea maendeleo wananchi.

Rais Mwinyi alisema mongoni mwa faida ya Muungano ni wananchi wa pande zote mbili wamekuwa wakifanya biashara ikiwamo ya mchele.

“Walaji wakubwa wa mchele ambao mwingi unatoka Tanzania Bara ikiwamo Morogoro wako Zanzibar, hivyo tuendelee kudumisha Muungano wetu kuhakikisha wananchi wetu wanapata fursa ya kuendelea kufanya biashara bila bughudha yoyote,” alisema.

Kuhusu miradi ya Jeshi Magereza, Dk Mwinyi alisema kwa mujibu wa Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, ni sehemu ya miradi mingi inayoendelea kutekelezwa na chombo hicho ndani ya mkoa huo na maeneo mbalimbali nchini.

Alisema hatua ya Jeshi la Magereza kuwa na ubunifu wa miradi mbalimbali ya maendeleo inafaa kuigwa kwa kuwa ni kielelezo kizuri kwa taasisi zingine kujiongeza na kujipatia kipato kutoka kwenye miradi yao pamoja na kuimarisha ustawi wa maisha ya wananchi ya kuwapatia huduma mbalimbali.

Nampongeza Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuiwezesha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia Jeshi la Magereza “ alisema.

“Nawapongezeni viongozi wa Jeshi la Magereza kwa usimamizi mzuri wa fedha za miradi hii kama tulivyosikia hivi punde karibu asilimia 75 ya fedha zinatoka serikali kuu kuiwezesha Magereza lakini asilimia 25 ni fedha za ndani ya jeshi jambo ambalo ni la kuingwa na taasisi zingine “ aliongeza.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alisema jeshi hilo limepewa jukumu la kujenga uwezo wa kujitengemea kwa chakula.

Simbachawene alisema Jeshi hilo kwa sasa lina uwezo wa kulisha wafungwa na mahabusi kwa asilimia 100 kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi sita na limeokoa takribani Sh. bilioni moja kwa mwezi ambapo kwa mwaka ni zaidi ya Sh. bilioni 12 zilizokuwa zinatolewa na serikali.

Pia alisema Jeshi hilo katika mikakati ya maboresho limejenga nyumba mpya za makazi ya askari na maofisa zipatazo 400 na nyingine bado zinaendelea kujengwa nchi mzima.

Habari Kubwa