Mwinyi kuweka mfumo maalum kwa wawekezaji

16Sep 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Mwinyi kuweka mfumo maalum kwa wawekezaji

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema iwapo atapata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar ataweka mfumo maalum kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika ukanda wa utalii kupewa kibali maalum, ili Wazanzibari waweze kunufaika.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kusini Unguja, wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi katika vijiji mbalimbali vya wilaya hiyo, alisema mfumo huo pia utakuwa maalum kwa wawekezaji hao, ili maeneo wanayonunua yanaendelezwe.

Alisema, maeneo mengi yamekuwa yakichukuliwa na wawekezaji hali ambayo inasababisha wananchi kukosa fursa za kujiajiri kupitia sekta hiyo.

"Wawekezaji tunawataka na kuwahitaji, lakini hatutaki kuona wanapewa ardhi bila ya kuuendeleza, akishindwa ananyang’anywa na kupewa mtu mwingine iweze kuendelezwa, ili serikali na wananchi waweze kunufaika," alisema.

Alisema, utalii ni sekta muhimu katika visiwa vya Unguja na Pemba ikiwamo fukwe, maeneo ya kihistoria na hoteli, hivyo serikali itaendeleza sekta hiyo kwa kuongeza idadi ya watalii wanaoiingia nchini kutoka 500,000 na kupokea zaidi ya 850,000.

Alisema serikali atakayoiongoza itaondoa dhuluma na upendeleo hasa katika upatikanaji wa ajira serikalini, ili kila Mzanzibari mwenye sifa ya kuajiriwa apate haki yake.

Alisema, atahakikisha suala hilo analifanyia kazi kwa umakini mkubwa na anafahamu changamoto zilizopo katika sekta hiyo serikalini.

Alisisitiza kuwa, amegombea nafasi hiyo kwa dhamira ya kuwatumikia Wazanzibari ikiwamo kusikiliza matatizo ya wananchi na kuyafanyia kazi.

Dk. Mwinyi, aliwataka wananchi kumwamini, kuona kazi hiyo na kazi nyingine anazifanya kwa nguvu na maslahi ya wananchi wa Zanzibar.

Pia alisema serikali ya awamu ya nane itaweka kipaumbele sekta ya uvuvi, ili iweze kuwanufaisha wananchi na bado Wazanzibar hawajanufaika na sekta hiyo.

Akizungumzia changamoto ya udhalilishaji, Dk. Mwinyi aliwahakikishia wananchi atashirikiana na wanajamii, ili kuunganisha nguvu za pamoja kuondoa tatizo hilo kabisa.

Aliahidi kuviwezesha vikundi vya ushirika kwa kuongeza mfuko wa uwekezaji, ili kinamama waweze kujiwezesha kiuchumi.

Kwa upande wao wananchi wa vijiji hivyo, walisema wana matumaini makubwa na Dk. Mwinyi katika kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwamo udhalilishaji wa wanawake na watoto katika jamii na sekta ya utalii, huduma ya upatikanaji wa majisafi na salama.

Mwananchi wa Kijiji cha Kizimkazi, Said Hamad Ramadhan, aliwaomba vijana kuacha kurubuniwa na watu, ambao hawana maslahi mema na nchi yao na badala yake kujenga uzalendo wa kuilinda, ili maendeleo yaweze kupatikana kwa haraka.

Habari Kubwa