Mwonekano, maisha mapya ya Ole Sabaya

19Oct 2021
Allan Isack
Arusha
Nipashe
Mwonekano, maisha mapya ya Ole Sabaya

MWONEKANO na maisha mapya ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, jana uliwachanganya mashahidi wa nne na wa tano kulazimika kuiomba Mahakama atoe barakoa ili wamtambue.

Tofauti na kabla ya hukumu ya Oktoba 15, mwaka huu, mshahidi waliofika mbele ya mahakama hiyo walimtambua kwa urahisi kwa kuwa mwonekano wake ulikuwa ni ule ule wa wakati akiwa kiongozi na kuonekana kwenye vyombo vya habari.

Jana Sabaya alitinga mahakamani humo akiwa amenyolewa upara ilhali mwonekano wake ni kunyoa panki, pia alinyolewa ndevu na kawaida yake ni mwenye ndevu maarufu kama mzuzu.

Mabadiliko hayo yamesababishwa na kuwa Sabaya kwa sasa ni mfungwa aliyehukumiwa jela miaka 30 baada ya Mahakama kumkuta na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Kwa mujibu wa taratibu za Magereza, mtu anapokuwa mfungwa hunyolewa kipara, na ndicho kilichotokea kwa Sabaya ambaye bado anakabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi na kutakiwa kuhudhuria mahakamani kila tarehe ya kesi husika.

Ole Sabaya na wenzake wawili Silvester Nyegu na Daniel Mbura, Oktoba 15, mwaka huu, walihukumiwa kifungo cha miaka 30 kwenda jela.

Katika kesi ya uhujumu uchumi mbali na Sabaya washtakiwa wenzake sita ni Silvester Nyegu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha (29), Nathan Msuya(31) wanakabiliwa na mashtaka matano.

Ilizoeleka kwa mshtakiwa huyo kunyoa panki na kuachia ndevu mithili ya mzuzu, lakini vyote hivyo jana havikuwapo kwa kuwa alikuwa amenyoa ndevu na nywele upara.

Mwonekano mpya wa Sabaya ulimfanya kuwa wa tofauti hadi mashahidi wa nne na wa tano katika kesi ya uhujumu uchumi walishindwa kumtambua hadi kuiomba mahakama washtakiwa hao kuvua barokoa ili waweze kuwatambua.

Awali, wakati wa kuanza kusikilizwa kwa kesi zote mbili ambazo ni ya jinai namba 105 na uhujumu, mshtakiwa huyo alikuwa akiwapungia waliofika mahakamani humo na kuongea mawili matatu na ndugu jamaa na marafiki.

 

Kwa siku ya jana hali ilikuwa tofauti kwa kuwa hakuwa na uchangamfu kama aliokuwa nao nyakati za nyuma, bali alipunga mara moja na kuingia mahakamani kwa upole.

Nyakati za nyuma alionekana kuwa na ujasiri jana hakuonyesha uso uliochangamka kama kawaida bali alijawa na huzuni.

Vile vile, mahudhurio ya watu katika kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi yamepungua ukilinganisha na kwenye kesi ya jinai iliyomalizika Oktoba 15, mwaka huu.

Pia, ndugu za washtakiwa hao wameonekana kutokuwa na furaha ukilinganisha awali kabla ya hukumu hiyo.

Habari Kubwa