Mzazi ajifungua 'famasi' afia juu ya bodaboda

27Jan 2017
Elisante John
SINGIDA
Nipashe
Mzazi ajifungua 'famasi' afia juu ya bodaboda

JESHI la Polisi Mkoa wa Singida, linawashikilia wanaume wawili kutokana na kifo cha mzazi aliyejifungua kwenye duka la dawa muhimu za binadamu (famasi) lililopo katika Kijiji cha Itagata wilayani Manyoni. 

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani humu, Debora Magiligimba, wanaoshikiliwa na jeshi hilo ni mume wa marehemu, Bahame Kamuda (32) na mmiliki wa duka hilo, Joseph Hengwe (50).

Kamanda Magiligimba alimtaja mzazi aliyefariki dunia baada ya kujifungua mtoto wa kiume dukani hapo kuwa ni Hellena Maduhu (29).  Mtoto wa marehemu yuko salama.

Alisema mzazi huyo alipelekwa dukani hapo na mume wake, Kamuda kwa lengo la kujifungua badala ya zahanati au hospitalini. 

Kamanda Magiligimba alisema awali mume wa marehemu na mke wake, walifika katika duka hilo kwa lengo la kujifungua, lakini ilibainika njia ya uzazi ilikuwa haijafunguka na wakashauriwa kwenda Hospitali ya Mt. Gasper iliyopo Itigi wilayani Manyoni. 
"Alianza kuhisi dalili za uchungu Januari 24," Kamanda Magiligimba alisema.

"Kesho yake saa tisa alasiri, alirudi tena na mumewe na kujifungua salama ila alianza kutokwa damu nyingi, hivyo mmiliki wa duka na mume wa marehemu, waliamua kumpeleka Itigi kwa usafiri wa pikipiki, lakini akafia njiani."

Kamanda Magiligimba alisema uchunguzi wa kitaalamu umebaini kifo cha mzazi huyo kimetokana na kuvuja damu nyingi baada ya kujifungua na siyo upasuaji unaodaiwa kufanywa kwenye duka hilo la dawa muhimu, kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Alisema pamoja na kuwashikilia watuhumiwa hao, jeshi hilo linaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na Idara ya Afya kubaini uhalali wa mmiliki wa duka hilo kutoa huduma ya uzazi kwa mwanamke huyo. 

Kamanda Magiligimba pia aliitaka jamii na wamiliki wa maduka ya dawa muhimu za binadamu kuwatilia mkazo elimu ya kuwawahisha kuwapeleka zahanati, vituo vya afya na hospitali wajawazito ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.  

Ripoti iliyotolewa mwaka jana na Benki ya Dunia (WB), inaonyesha kuna wastani wa vifo 1,255 vitokanavyo na uzazi nchini kila mwezi, sawa na vifo 42 kila siku na viwili kila saa, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni mazingira duni ya kujifungulia.

 

Habari Kubwa