Mzee asotea mafao mwanawe miaka minne

09Oct 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Mzee asotea mafao mwanawe miaka minne

MZEE Ismail Nguvu (75), ameliomba Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kulipa mafao ya mwanawe Nasibu Nguvu, aliyefariki dunia mwaka 2016.

Kijana huyo ambaye alikuwa mchangiaji kwenye mfuko wa PPF uliounganishwa na NSSF mwaka jana, alikuwa mwanachama wa mfuko huo namba 2320865 ambaye alichangia Sh. 4,874,970.72. Nasibu alikuwa mfanyakazi wa hoteli ya Holday Inn jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam, alisema wameshafuatilia mara nyingi kabla ya mifuko kuunganishwa hadi inaunganishwa bila mafanikio.

Alisema mwanawe ameacha mke na watoto na walitarajia fedha hizo zitatumika kuwasomesha lakini kila siku wanapigwa danadana.

"Mwanangu unavyoniona hapa mimi ni mgonjwa, lakini hakuna mtu wa kufuatilia haki ya mwanangu. Kila nikifuatilia zilipokuwa ofisi za PPF na baadaye NSSF naambiwa faili lake lipo kwenye hatua nzuri," alisema.

"Tumefuatilia sana, tunaambiwa tusubiri hundi ambayo imetumwa kwenye akaunti ya msimamizi wa mirathi. Sasa ni miezi 15 sasa hakuna mafanikio yoyote," aliongeza.

Alisema kijana wake alichangia mfuko huo akiamini kama kutatokea tatizo lolote katika maisha yake fedha hizo zitasaidia kama ilivyotokea kifo lakini fedha zake hazijulikani zilipo na mifuko haitoi majibu sahihi.

"Miezi 15 bila mafanikio zimeliwa au amepewa mtu mwingine anayehusika au zimekopeshwa kwa watu hawajarudisha? Mimi ni baba mzazi wa marehemu umri wangu naelekea miaka 80 sasa. Naomba kujua tatizo liko wapi kwenye kuandika hundi au kuna jambo lingine?" Alihoji.

Barua kutoka Holiday Inn, yenye kumbukumbu namba EMPL/HOL/CODE.029/16, kutoka kwa Meneja Rasilimali Watu kwenda kwa familia, kuhusu kuthibitisha kifo cha kijana huyo, ilieleza kuwa kijana huyo alianza kufanya kazi Machi Mosi, 2013.

Katika barua hiyo, imeelezwa kuwa michango ya mwanachama huyo ilikuwa ikipelekwa PPF.

Ripoti ya uchangiaji kutoka PPF, ilionyesha kuwa alianza kuchangia Juni, 2013 alichangia Sh. 55,424 kiwango ambacho kiliongezeka kwa kadri mshahara ulivyoongezeka na hadi anafariki dunia alikuwa analipwa Sh. 600,000 na mchango wake kwenye mfuko ilikuwa Sh. 120,000 kwa mwezi na kufanya jumla ya michango 42.

Ripoti hiyo ilichapishwa Agosti 20, 2018 na mtumishi wa mfuko huo aitwaye Hsabaya.

Kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii, iwapo mwanachama atafariki dunia, michango yake wanapewa warithi wake na iwapo atafariki dunia baada ya kufikisha miezi 180 ya uchangiaji warithi wake watalipwa mkupuo na pensheni ya kila mwezi kwa miezi 36.

Habari Kubwa