Mzigo fao kujitoa waanikwa

14May 2018
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mzigo fao kujitoa waanikwa

SERIKALI imefuta fao la kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii nchini, ili kuepuka kuja kuwa na wazee ambao ni mzigo kwa taifa la baadaye.

Meneja Mawasiliano wa NSSF, Salim Kimaro.

Aidha, Sheria ya Mifuko ya Jamii ya Mwaka 2017 ambayo imeunganisha taasisi hizo imelenga kupanua wigo wa sekta hiyo na kutoa mafao bora.

Meneja Mawasiliano wa NSSF, Salim Kimaro, alisema hayo katika mazungumzo na Nipashe mwishoni mwa wiki, iliyotaka kujua maendeleo ya utayarishaji wa kanuni za fao jipya la ukosefu wa ajira kwa wanachama wake.

Kimaro alisema wakati serikali ikilenga kuunganisha mifuko hiyo, dhamira ilikuwa ni kupanua wigo wa hifadhi ya jamii, kutoa mafao bora na kuwa taifa lenye wazee wenye hifadhi ya jamii ambao hawatakuwa mzigo kwa taifa.

Dhamira ya serikali kuwa na taifa lenye wazee wasio tegemezi haitatimia endapo watumishi wanaoacha au kuachishwa kazi watakimbilia kuchukua fedha zao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, alisema Kimaro.

“Ili mtu aweze kuwa na sifa ya kupata mafao ya kustaafu inalazimika awe na sifa maalum ambazo ni awe amechangia kwa miaka 15 na awe amefikia umri wa miaka 60 kwa lazima ama miaka 55 kwa hiyari,” alifafanua.

Kimaro alisema mtumishi aliyefanyakazi kwa miaka kadhaa na kuchukua fedha zake, anapopata kazi sehemu nyingine huanza upya uanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii hivyo ni vigumu kufikia sharti la kuchangia kwa miaka 15, ili kupata pensheni.

“Ndiyo maana mashirika ya hifadhi ya jamii, ikiwamo NSSF yanashinikiza na kueleza watu wanapoacha kazi wasikilimbilie kutoa fedha zao ila waache; wakipata ajira sehemu nyingine waweze kuendeleza michango yao,” alisema Kimaro.

“Hata wasipopata ajira za kuajiriwa wanaweza kuendelea kuchangia wenyewe kwa mfumo wa hiyari hadi wapate sifa ya pensheni kwa mfumo huo.

"Hakuna sababu ya mtu kukimbilia kuchukua fedha... inamharibia namna ya michango na kumfanya ashindwe kupata pensheni na hiyo siyo dhamira ya serikali au mashirika ya hifadhi ya jamii.”

Alisema hivyo Sheria ya Mifuko ya Jamii ya Mwaka 2017 iliyopitishwa na Bunge mwanzoni mwa mwaka na kusainiwa na Rais John Magufuli Februari ni suluhisho kwa kuwa imekuja na fao la kukosa ajira.

“Hadi sasa miongozo inaandaliwa ambayo itafafanua namna ambavyo fao hili litakavyotolewa kwa mifuko miwili itakayobaki ambayo ni NSSF na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).”

Mbali na kuanzisha fao jipya kwa watumishi ambao watapoteza ajira, sheria hiyo pia imeunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kubaki miwili -- mmoja wa sekta binafsi na mwingine sekta ya umma.

Mifuko ya GEPF, PSPF, PPF na LAPF imeunganishwa kuwa PSSSF kwa upande wa umma na NSSF kwa sekta binafsi na mashirika ya kimataifa.

Ilielezwa bungeni mjini Dodoma mapema mwaka huu kuwa wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi kwenye mifuko ya GEPF, PSPF, PPF na LAPF, watapata ajira katika mfuko mpya wa PSSSF, isipokuwa wachache wasio na maadili au hawaendani na mfumo wa mifuko hiyo.

Akitoa takwimu za idadi ya wafanyakazi katika mifuko ya umma na sekta binafsi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alisema kwa mujibu wa takwimu za Septemba, mwaka jana kulikuwa na jumla ya wafanyakazi 2,147 wanaohudumia wanachama na wastaafu 1,404,461.

Waziri Mhagama alisema mfuko mpya wa PSSSF utachukua wafanyakazi 988 kutoka kwenye mifuko hiyo minne inayounganishwa, na mfuko wa NSSF unahitaji wafanyakazi 1,159.