Mzizi wa fitina utata vichwa treni wakatwa

14Sep 2017
Romana Mallya
Nipashe
Mzizi wa fitina utata vichwa treni wakatwa

WAKATI kukiwa na utata wa vichwa 11 vya treni vilivyokamatwa katika Bandari ya Dar es Salaam, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imesema imepata vielelezo vyote kuhusu suala hilo na kumtaja mmiliki.

Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni nchini juzi, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, alisema mbali ya kupata vielelezo hivyo, wamewahoji watuhumiwa na wadau wote wanaohusika na suala hilo.

Vichwa hivyo 13 vya treni vilikamatwa mwezi uliopita wakati Rais John Magufuli alipofika bandarini hapo kwa ajili ya hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya upanuzi wa ujenzi wa bandari ya Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema ana taarifa ya uwapo wa vichwa 11 vya treni bandarini hapo ambavyo mmiliki wake hajulikani na inaelezwa ni vibovu.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, alisema vichwa hivyo vina nembo ya
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na ulitokea mgogoro kati ya TRL na kampuni iliyotengeneza baada ya kubainika mchakato mzima wa manunuzi haukuwa sahihi.

TRL ilinunua vichwa 15 vya treni kutoka kampuni ya EMD (Electro-Motive Diesel) ya Marekani na utengenezaji wake ukafanywa na Kampuni ya DCD ya Afrika Kusini.

Baada ya kusaini mkataba huo, Machi mwaka 2015 TRL ilipokea vichwa viwili vya treni na hivyo vilibaki vingine 11 ambapo ununuzi huo uligharimu Sh. bilioni 70.5, fedha ambazo zililipwa na serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRL, Machi 23, mwaka 2015, ununuzi huo wa vichwa vya treni ulikuwa ni mpango wa serikali wa kuifufua TRL chini ya mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Akizungumzia kuhusu uchunguzi wa vichwa hivyo na hatua wanazozichukua juzi, Mlowola alisema kwenye uchunguzi kuna vitu viwili, ama unaweza kukuta taratibu za kiutawala zilikiukwa au makosa ya jinai yalitendwa.

“Bado tunaangalia sababu, ili kujua nini kilifanyika kwa kuwa tayari watuhumiwa, wadau wote wahusika wote wameshahojiwa, vielelezo vyote vimeshapatikana,” alisema.

Aliongeza, “kama kutakuwa na hatua za kijinai tukimaliza uchunguzi tutapeleka jalada kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali akibaini kuna makosa ya kijinai na yanaweza kuthibitishwa ndipo tunakwenda mahakamani.”

Akielezea zaidi, Mlowola alimtaja mmiliki wa vichwa hivyo ni kampuni ya Electro-Motive Diesel ya Marekani.

Alisema wamebaini mchakato wa kununua vichwa hivyo ulianza mwaka 2014/15, lakini hawakufika mwisho na hapakuwa na mkataba wa vichwa hivyo kufikishwa nchini au kununuliwa nchini.

“Shirika linalohusika na usafirishaji wa reli lilianza mchakato wa manunuzi ya vichwa hivi, lakini hapakuwa na mkataba wa mauziano kwa hiyo hawa walileta kwa matumaini vitanunuliwa,” alisema.

Alisema kampuni hiyo ilileta nchini vichwa hivyo, lakini hapakuwa na mkataba wa makubaliano wa mauziano baina yao na TRL.

Katika mahojiano hayo, Mlowola alizungumzia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Takukuru kuhusu ripoti mbili za Kamati Maalum ya Bunge zilizochunguza mfumo wa uchimbaji, usimamizi na biashara ya madini ya Almasi na Tanzanite na kueleza uchunguzi ulianza mara moja baada ya Rais kuvikabidhi vyombo vya ulinzi na usalama ripoti hizo kwa hatua zaidi dhidi ya waliotajwa ndani yake.

Habari Kubwa