Nabii Suguye asikitishwa watumishi wa Mungu wanaodai kutibu Corona

17Feb 2020
Mary Geofrey
DAR
Nipashe
Nabii Suguye asikitishwa watumishi wa Mungu wanaodai kutibu Corona

ASKOFU na Nabii wa Kanisa la Huduma ya Neno la Upatanisho (WRM), Nicolaus Suguye, amesema anasikitishwa na watumishi wa Mungu wanaodai wanaweza katibu ugonjwa wa Virusi vya Corona.

ASKOFU na Nabii wa Kanisa la Huduma ya Neno la Upatanisho (WRM), Nicolaus Suguye.

Amewataka watumishi nchini kuacha kujiingiza kwenye suala hilo linalogharimu maisha ya watu wengi na badala yake wafanye maombi na kuacha kutafuta umaarufu kupitia matatizo ya watu.

Askofu Suguye aliyasema hayo jana Jijini Dar es Salaam, wakati wa sherehe ya kuadhimisha miaka 13 tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo nchini, ziilizofanyika katika kanisa hilo lililopo Kivule wilayani Ilala.

"Jambo linalonisikitisha ni kuhusu tishio la mgonjwa wa Corona, baadhi ya watumishi wanaibuka na kusema wana dawa na wanaomba ndege ya kuwapeleka kwenda China kutoa tiba. Naomba watumishi wenzangu kama hawana tiba waache kutafuta umaarufu kupitia tatizo hilo kubwa," alisema Suguye.

Hivi karibuni, aliibuka mtumishi wa Mungu aliyedai anatiba ya virusi vya Corona huku akiomba msaada wa ndege kwenda kutoa tiba nchini China.

Hadi jana watu 20,438 waliripotiwa kuambukizwa virusi vya Corona nchini China.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Tume ya taifa ya afya nchini China, watu 64 walifariki dunia katika jimbo la kati la Hubei, sehemu ambayo ugonjwa huo ulianzia na kufanya idadi ya jumla ya watu waliofariki kufikia  425.

Mbali na hilo, Askofu Suguye aliwataka Watanzania kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kuduma la wapiga kura hususani wakazi wa Dar es Salaam ambao wanaendelea kujiandikisha ili kushiriki kupiga kura kuchagua viongozi wanaostahili kuwaongoza.

Alisema suala la uchaguzi ni la kusimama pamoja kama kanisa na Watanzania kuomba kwa ajili ya kupata viongozi bora watakaosimama kuongoza kwa miaka mingine mitano.

Aidha, aliwataka Watanzania kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wote wa uchaguzi kwa sababu inawafanya washindwe kuchagua viongozi wanaofaa kuwaongoza.

Naye Nabii wa Huduma ya Calvary Assemblies of God, Danstan Maboya, aliwataka Watanzania kuendelea kumuomba Mungu kwa ajili ya uchaguzi mkuu ufanyike kwa amani na utulivu.

Alisema suala la uchaguzi siyo la dini wala kabila na kwamba linapaswa kusimamiwa na Watanzania wote kwa maslahi mapana ya Taifa

Habari Kubwa