Naibu IGP aonya vitendo vya aibu ndani ya polisi

23Sep 2016
Ibrahim Joseph
Nipashe
Naibu IGP aonya vitendo vya aibu ndani ya polisi

Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Inspekta Jenerali Abrahaman Kaniki, amepiga marufuku uvaaji wa sketi fupi kwa askari wa jeshi hilo.

Sambamba na hilo, amewaonya viongozi wa jeshi ambao wamekuwa wakivunja taratibu ikiwamo kuwa na uhusiano wa kimapenzi na askari wa chini kwa kuwa hiyo ni sawa na kumkabidhi mtu kondoo kuwachunga na badala yake anawala.

Pamoja na marufuku hiyo, Kaniki amewataka makamanda na maofisa waandamizi wa jeshi hilo, kupiga vita tabia ya baadhi ya askari wanaovaa sare kinyume cha maadili ya jeshi.

Akifungua kongamano la siku tatu la mtandao wa polisi wanawake nchini, mjini hapa jana, alisema uvaaji wa sare za jeshi hilo uliopigwa marufuku hautakiwi na kwamba atakayebainika atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Aliyataja baadhi ya mavazi yasiyoruhusiwa kuwa ni pamoja na uvaaji wa suruali chini ya kiuno, maarufu kama ‘kata k’ kwa askari wa kiume na sketi fupi kwa askari wa kike.

Kaniki alisema mitindo ni kinyume cha maadili ya jeshi, hivyo kuanzia wiki ijayo makamanda wa mikoa, vikosi na wilaya wanapaswa kusimamia na watakaoshindwa kuwadhibiti watawajibishwa.

“Kwenye hili ninawaambie bahati mbaya sina la kuficha. Hamwezi kukwepa lawama za hili. Kamishna Alice Mapunda lichukue hili na lijadiliwe kwa makini humu kwenye kongamano lenu, mje na maazimio mmejipangaje,” alisema.

Alisema jeshi hilo limeanzisha kamisheni ya intelijensia na moja ya majukumu yake ni kutoa taarifa za uvaaji sare kwa askari wote.

Kuhusu askari wa kike wanaovaa kinyume cha utaratibu, kiongozi wa eneo atakuwa na kesi ya kujibu na kwamba msimamizi pia atahusika.

Kaniki alisema askari wa kike wanatakiwa kuvaa sketi zinazovuka chini ya magoti watakaoshindwa kufanya hivyo wataonekana kushindwa kutii agizo hilo na kuongeza kuwa kuanzia wiki ijayo, baada ya semina hiyo watahitaji taarifa za uvaaji wa askari wote hasa wa kike kwa kuwa watakuwa wamepata taarifa za matokeo ya mafunzo hayo.

Katika hatua nyingine, Kaniki alionya tabia ya baadhi ya wakuu wa vikosi kutowalinda askari wa chini badala yake wanawafanya kuwa mawindo akimaanisha tabia ya kuchanganya mapenzi na kazi.

“Tusichanganye mawindo na kazi. Msisite kutuletea taarifa zao kwa kuwa hatuwezi kuendelea na tabia hizo kazini na wale wanaofanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua,” alisema.

Naye Mkuu wa Mtandao wa Polisi Wanawake, Kamishna Alice Mapunda, aliwataka moafisa wa kike kuchangamkia fursa ya kujiendeleza kielimu ili kuchukua nafasi za juu katika jeshi hilo.

Hata hivyo aliwaasa kuaachana na kasumba za kufikiria kuwa vyeo vya juu vya polisi vinatolewa kwa upendeleo.

Habari Kubwa