Naibu Meya wa zamani afikishwa mahakamani

23Sep 2016
Cynthia Mwilolezi
Nipashe
Naibu Meya wa zamani afikishwa mahakamani

NAIBU Meya wa zamani wa jiji la Arusha kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Diwani wa sasa wa Kata ya Daraja Mbili mjini hapa, Prosper Msofe amefikishwa mahakamani na mwenzake mmoja kujibu mashtaka matatu likiwamo la kujipatia Sh. milioni nane kwa njia ya udanganyifu.

Fedha hizo, imedaiwa, zilikuwa zitumike kwenye mradi wa maji. Mshtakiwa mwenza wa Msofe ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya Daraja Mbili, Modestus Lupogo.

Washtakiwa walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na kusomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mfawidhi Augustine Rwizile.

Wakili wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha, Monica Kijazi, alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda makosa hayo Oktoba na Novemba, mwaka 2013.

Wakili Monica alidai kuwa mtuhumiwa Lipogo akiwa Ofisa Mtendaji wa Kata, anatuhumiwa kuwasilisha nyaraka za uongo akionyesha bajeti ya mapato na matumizi katika kipindi cha Oktoba na Desemba, 2013.

Alidai kuwa mtuhumiwa huyo alionyesha Sh. milioni nane zimetumika kwenye mradi wa maji katika mtaa wa Alinyanya na Sanare Kata ya Daraja Mbili.

Wakili Monica aliwasomea kosa la pili watuhumiwa wote akidai kuwa kwa pamoja wanadaiwa kushiriki kutenda kosa la ubadhirifu wa fedha za umma.

Katika shtaka la tatu, washtakiwa wanadaiwa kufanya matumizi binafsi badala ya yaliyokusudiwa katika fedha za umma na kujipatia Sh. milioni nane kupitia nafasi walizokuwa nazo.
Hata hivyo, washtakiwa walikana mashtaka hayo na kuachiwa kwa dhamana.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 10, mwaka huu washtakiwa watakaposomewa maelezo ya awali.

Habari Kubwa