Naibu Spika aipongeza CRDB riba nafuu mikopo wanawake

03Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Naibu Spika aipongeza CRDB riba nafuu mikopo wanawake

NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ameipongeza Benki ya CRDB kwa kupunguza riba kwa mikopo ya wanawake wajasiriamali.

Mikopo hiyo inapatikana kupitia huduma ya “CRDB Malkia” hadi kufikia asilimia 14 kwa mwaka.

Akizungumza katika uzinduzi wa CRDB Malkia, Dk. Tulia alisema hatua ya benki hiyo kupunguza riba kwa asilimia 10 kutoka asilimia 24 iliyokuwa ikitozwa mwanzo, itasaidia wanawake wengi zaidi kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo.

“Kupungua kwa riba ina maana inapunguza mzigo mkubwa wa marejesho kwa wanawake na kuwafanya kuwa na fedha nyingi kwa ajili ya uwekezaji katika biashara zao, hivyo kupelekea kufanikisha zaidi,” alisema Dk. Tulia.

Aisema pamoja na utafiti kuonyesha wanawake wamekuwa na ushiriki mkubwa katika shughuli za uchumi nchini, kwa asilimia 54, ni asilimia 60 tu ya wanawake ndio wenye kufikiwa na huduma rasmi za kifedha.

“Niwapongeze pia kwa kuboresha masharti ya dhamana ili kutoa fursa kwa wanawake wengi zaidi kuweka mikopo,” aliongezea Dk. Tulia, huku akiwataka wanawake pia wajitokeze kwa wingi kufungua akaunti ya Malkia itakayosaidia kufanikisha malengo yao kwa kujiwekea akiba kidogokidogo, jambo litakalosaidia kujenga imani kwa taasisi za fedha.

“Mimi ni mmoja wa wanawake waliofungua akaunti ya Malkia wakati ikianzishwa mwaka 2009, nimefurahi kuona leo hii Benki yetu ya CRDB ikifanya maboresho yatakayoweza kumkomboa mwanamke.”

Dk. Tulia alisema jitihada hizi zinazofanywa na Benki ya CRDB katika uwezeshaji wa makundi mbalimbali ya wananchi zimekuwa na msaada mkubwa katika kuisaidia Tanzania kufikia lengo la kuwa nchi yenye uchumi wa kati.

“Nimefurahi kuona leo hii tukiwa tunajivunia kuwa nchi ya uchumi wa kati, Benki yetu ya CRDB inaendelea kutubeba wanawake na kuwezesha kufikia malengo yetu ya nchi na dunia katika kuwa na usawa katika ushiriki katika shughuli za maendeleo kama ilivyoainishwa katika mpango wa Maendeleo Endelevu 2030 wa Umoja wa Mataifa,” alisema Dk. Tulia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema huduma ya CRDB Malkia imelenga katika kumtambua, kumpa nafasi na kumwezesha mwanamke wa Kitanzania kufikia malengo yake kupitia mikopo ya biashara na ujasiriamali, kujiwekea akiba kwa akaunti ya Malkia na mafunzo ya uendeshaji biashara.

“Mpaka kufikia mwishoni mwa Machi mwaka huu, benki yetu tayari ilikuwa imeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 600 kwa wanawake zaidi ya 55,000,” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa zaidi ya wanawake 30,000 wameshajiunga na akaunti ya Malkia.

Habari Kubwa