Naibu Waziri adaiwa kutoa rushwa kura za maoni UWT

05Aug 2020
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Naibu Waziri adaiwa kutoa rushwa kura za maoni UWT

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Mary Mwanjelwa, amedaiwa kutoa rushwa kwa wajumbe wa Mkutano wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Mbeya ili achaguliwe kuwa mgombea ubunge wa viti maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Mary Mwanjelwa:PICHA NA MTANDAO

Ujumbe unaodaiwa kuwa wa kiongozi huyo, umesambaa mitandaoni akielezea fedha alizotoa kwa wajumbe zilivyoliwa na viongozi kutoka moja ya wilaya za mkoa huo.

Kutokana na tuhuma hizo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema inafuatilia tuhuma hizo kabla ya kuchukua hatua.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema taasisi yake imepokea ujumbe huo na inaufanyia kazi.

“Ujumbe huo tumeupata na tayari tunaufanyia kazi na majibu yake mtaambiwa,” alisema kwa kifupi Jenerali Mbungo.

Kwa upande wake, Mwanjelwa alipopigiwa simu kuthibitisha kama sauti hiyo ni yake, hakukubali wala kukataa, zaidi ya kusema yuko kwenye kikao.SAKATA ZIMA

Ujumbe huo ambao ulianza kusambaa jana asubuhi kwenye mitandao ya kijamii unamkariri Mwanjelwa akihoji kwa nini baadhi ya wajumbe hawakupewa fedha alizotoa kwenye uchaguzi huo.

Kwenye ujumbe huo, Mwanjelwa anasikika akimkaripia Katibu wa UWT Wilaya ya Mbarali aliyefahamika kwa jina la Vero, ambaye anadaiwa alipewa Sh. 100,000 kwa ajili ya kumpa kila mjumbe lakini yeye akapunguza na kutoa Sh. 50,000.

Hata hivyo, Mwanjelwa alisikika akisema mpaka kufikia jioni kuamkia siku ya uchaguzi, hakuwa na nia ya kutoa fedha lakini aliambiwa na wapambe wake kuwa asipotoa mambo yanaweza kuwa magumu kwake kwa sababu wenzake wanatoa.

Mtu aliyefahamika kwa jina la Zabibu, anayedaiwa kuwa Mwenyekiti wa UWT Wilaya, akimweleza Mwanjelwa kwamba Katibu hakuwapa wajumbe mzigo alioutoa na badala yake amewapa watu aliowataka tu.

“Wajumbe kibao hajawapa na mimi nimempigia sasa hivi nimemwambia mbona wale watu hujawapa akaniambia hela zilikuja chache nikamwambia hapana,” alisema Mwenyekiti huyo huku Mwanjelwa akisikika kwamba fedha zilipelekwa kwenye bahasha zikiwa zimehesabiwa maalum kwa wajumbe, hivyo hakuna uwezekano wa kupotea.

“Naijua Mbarali iko kwenye vidole vyangu. Wajumbe wenyewe nawajua kama navyojua mboni ya jicho langu, najua wako wangapi, kama ni mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa, mjumbe wa mkutano mkuu wa wilaya, makatibu nawajua na najua kata ziko ngapi,” alisikika Mwanjelwa akizungumza na mtu huyo.

“Kwanza haitakiwi ijulikane kwamba kuna hela ilikuja kutoka kwangu. Mimi nampigia atoe hela maana italeta maneno, watu wamemwaga mahela sana, watu wanajua na fedha niliyotoa ni halali na nilifanya hivyo baada ya kuona watu wametoa hela, yaani watu wamemwaga mahela mpaka basi,” alisikika akisema.

Mwanjelwa pia alisikika akisema kutoa hela hizo ilikuwa haki yake na hana kawaida ya kubagua watu kwa kuwa hata wale waliokuwa wanamchukia kwenye uchaguzi huo alitaka wote wapate mgawo bila kubaguliwa.

Baada ya mazungumzo hayo, Mwanjelwa alimpigia Vero na kumhoji kwa nini hakutoa mgawo kama ulivyokuwa umepangwa kwa wajumbe. Sehemu ya mazungumzo hayo ilikuwa kama ifuatavyo;-

Mwanjelwa: Dada hujambo.

Katibu:  Sijambo

Mwanjelwa: Sasa sikiliza nikwambie mdogo wangu, mwenyekiti amenipigia sasa hivi.

Katibu: Na mimi nilikutumia ujumbe kwenye simu jana.

Mwanjelwa: Meseji yako sijaiona lakini mzigo ulioletewa wote ulikuwa umekamilika kwa sababu Mbarali yote naifahamu iko kwenye vidole. Niliandika madiwani wanne, nikaweka ya kwako na ya mwenyekiti.

Vero: Mimi nilipokea bahasha nikiwa sina gari nikagawa nikagawa wee zikapelea nikasema nimwite mwenyekiti nimweleze.

Mwanjelwa: Hapana, hapana. Haiwezekani bahasha zikapelea Vero wakati zilihesabiwa jamani.

Vero: Sasa mimi sijui hapo imekuwaje.

Mwanjelwa: Ngoja nikueleza wengine hujawapa italeta maneno wape bahasha zao wote  wewe si uliniambia una kata 24 kwa hiyo mimi nikapiga hesabu ya kata 24 mara mbili ukichukua Mwenyekiti wa Wilaya, Katibu wa Wilaya, madiwani wanne na mjumbe wa halmashauri kuu na tena niliandika hadi kikaratasi sasa zinapelea wapi Vero au ina maana wale niliowatuma ndio walionyofoa?

Katibu: Yaani mimi sijajua au wakati ule nagawa kuna watu walipokea mara mbili sijajua.

Mwanjelwa: Yaani hiyo italeta maneno inabidi ulitengeneze hilo jambo kwa sababu watu walishajua kwamba kuna mzigo wao ulikuja.

Katibu: Najua kweli italeta shida.

Mwanjelwa: Ni kweli italeta shida na itakuharibia sana

Katibu: Sasa mimi sijui nitaliwekaje kwa kweli.

Mwanjelwa:  Hiyo sasa itakuharibia kwanza haitakiwi ijulikane kwamba kuna bahasha zilikuja kutoka kwangu semeni kuna mgombea alileta.

Katibu: Mimi wale waliokosa niliwaambia subirini.

 Mwanjelwa: Sasa wasubiri utawalipaje wakati bahasha zililetwa zote. Na unadhani kuna mtu atakuamini hapo si wataona umezinyofoa? Hata mimi naona umezinyofoa kwa sababu yule mtu niliyemtuma ni wa ndani ya familia na alipokuja pale alithibitisha kukupa bahasha zote.

Mimi sitakubali ijulikane kwamba kuna bahasha zangu zilikuja kwako hapana sitakubali kabisa hilo litakuharibia wewe, mimi nitakuruka kimanga sitakubali liniletee sura mbaya nitakuruka mimi.

Katibu: Sijui kuna waliochukua bahasha mbilimbili lakini hata kama walichukua hawawezi kusema.

Mwanjelwa: Sasa si uzembe uliufanya wewe, fedha zilikuja kwenye bahasha zikiwa zimefungwa zingekuwa hazijafungwa tungesema labda ulikosea kwenye kuhesabu, lakini hazikuwa wazi na bahasha ndizo zilizokuwa zikihesabiwa sio hela sasa ulikoseaje.

Katibu: Inawezekana wakati wa kutoa nikakosea na kuwapa wengine bahasha mbili mbili.

Mwanjelwa: Hapana Vero. Sikiliza, hivi inawezekaje kumpa mtu bahasha mbili mbili wakati zinaonekana. Mdogo wangu Vero najua fedha ni shetani  lakini pesa yangu haiwezi kupotea hivi hivi. Naomba uongee na mwenyekiti mlitengeneze.

Baada ya mazungumzo na Katibu anayetuhumiwa kuchoka fedha hizo, Mwanjelwa alirudi kuzungumza na mwenyekiti na kuhoji kuwa katibu alikuwa akigawa fedha hizo kwa kutumia kigezo gani.

Mwanjelwa alisikika akisema kuwa kama kuna wajumbe ambao hawakuwapo wakati mgao huo ukitolewa mhusika alipaswa kuwawekea au kuwapa viongozi wenzao.

Mwenyekiti huyo alimweleza  Mwanjelwa kwamba kuna karibu kata 10 ambazo  hazikufikishiwa mgawo huo hivyo huenda Katibu akawa amebaki na zaidi ya Sh. milioni tatu.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wa chama ambao kutokana na kukosa mgawo huo walitishia kutopeleka wajumbe kupiga kura wakati wa uchaguzi wa viti maalum kwa upande wa madiwani.

Habari Kubwa