Naibu Waziri akerwa bajeti kiduchu ya ardhi halmashauri

19Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Rufiji
Nipashe
Naibu Waziri akerwa bajeti kiduchu ya ardhi halmashauri

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula, ameelezea kukerwa na tabia ya wakurugenzi wa halmashauri nchini kwa kuzitengea fedha kidogo idara za ardhi, hivyo kuzifanya kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo.

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula, picha mtandao

Akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani jana, Mabula alisema wakurugenzi wengi katika halmashauri wamekuwa wakiifanya idara ya ardhi kama mtoto yatima.

‘’Ukienda katika halmashauri nyingi idara ya ardhi imekuwa kama mtoto yatima na ofisi zake haziridhishi kabisa kulinganisha na zile ofisi za idara zingine kama vile afya na elimu’’ alisema.

Kwa mujibu wa Mabula, katika halmashauri nyingi alizotembelea, bajeti katika idara za ardhi haizidi Sh. milioni nne tofauti na fedha za mapato ya ndani ingawa wakati mwingine hazipatikani zote.

Alisema tatizo linaloonekana ni wakurugenzi kutofahamu kama idara hiyo ina fedha nyingi na kuweka wazi kuwa iwapo halmashauri zitaamua kuisimamia sekta hiyo kikamilifu, zitajikusanyia mapato mengi kulinganisha na sekta zingine.

Mabula alisema katika ukusanyaji mapato ya serikali nchini, sekta ya ardhi inaweza ikawa sekta ya pili au ya tatu kwa kuingiza mapato mengi ikiwa nyuma ya taasisi zinazokusanya mapato moja kwa moja kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Mashaka Abdallah, alimweleza Mabula kuwa idara yake inakabiliwa na ufinyu wa bajeti inayotengewa kwa ajili ya kutekeleza kazi za ardhi na vitendea kazi kama kompyuta, mashine za uchapaji na usafiri.

Alisema katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 halmashauri yake ilipangiwa kukusanya Sh. milioni 15 na hadi Desemba 31, mwaka jana ilishakusanya Sh. milioni 16.7 ikiwa ni sawa na asilimia 111.6.

Kutokana na maelezo hayo, Mabula alisema ukosefu wa vitendea kazi unawakatisha tamaa watendaji wa sekta hiyo lakini pia unachangia watendaji hao kutofanya kazi vizuri na wakati mwingine kuwalazimu kutumia fedha zao za mfukoni kufanikisha kazi walizopangiwa.

Kuhusu ukusanyaji mapato kupitia sekta ya ardhi, Mabula alisema halmashauri nyingi zimekuwa zikifanya makisio kidogo ya fedha za makusanyo huku zikiacha fedha nyingi kwa wadaiwa na kuwataka watendaji kuweka makadirio kulingana na uhalisia wa madeni wanayodai.

Alitolea mfano wa halmashauri ya wilaya ya Rufiji kuwa pamoja na kuwekewa kiwango cha kukusanya Sh. milioni 15, ilikusanya Sh. milioni 16.7 kujivunia kuvuka lengo lakini kumbukumbu zilizoko wizarani zinaonyesha halmashauri hiyo inadai zaidi ya Sh. bilioni moja.