Naibu Waziri amtega ofisa ardhi

16Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Kyerwa
Nipashe
Naibu Waziri amtega ofisa ardhi

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula amempa wiki moja Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kuhakikisha anaingiza viwanja 516 katika mfumo wa malipo ya serikali kwa njia ya kielektroniki vinginevyo ataondolewa katika wadhifa huo.

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula picha mtandao

Agizo hilo limetolewa baada ya Mabula kuelezwa na mkuu huyo wa idara kuwa, katika halmashauri hiyo viwanja 348 pekee ndivyo vilivyoingizwa katika mfumo wa malipo wa kielektroniki huku viwanja 516 vikiwa havijaingizwa.

Mabula alitoa agizo hilo jana akiwa katika mfululizo wa ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi katika wilaya za mkoa wa Kagera.

Alisema kuna uzembe mkubwa kwa mkuu huyo wa idara ya ardhi ambaye pia ni ofisa ardhi mteule wa halmashauri katika kusimamia uingizaji viwanja kwenye mfumo ambao ndio unaosaidia kuongeza mapato ya serikali.

Naibu Waziri alishangazwa na mkuu huyo kushindwa kuingiza idadi hiyo ya viwanja kwenye mfumo huo katika kipindi cha mwaka mzima wakati alieleza kuwa kwa siku moja anao uwezo wa kuingiza viwanja ishirini.

‘’Kuna uzembe katika kusimamia idara hii ya ardhi na kama mzigo ni mkubwa kwako kusimamia idara hii basi chagua kuachia nafasi moja kati ya ukuu wa idara ya ardhi au ofisa ardhi mteule ili kuifanyia nafasi moja kwa ufanisi,’’ alisema Mabula.

Kuhusu utoaji hati, Mabula aliiagiza halmashauri kuhakikisha maeneo yote yaliyochukuliwa kwa ajili ya matumizi ya umma yanapatiwa hati ili kuepuka migogoro ya ardhi.

Alisema migogoro mingi kwenye taasisi za umma inasababishwa na taasisi hizo kutokuwa na hati kwenye maeneo yake na kutolea mfano moja ya maeneo yanayovamiwa sana ni yale ya wazi na kuzitaka  idara husika kusimamia suala hilo kwa makini.

Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Rashid Mwaimu, alisema viwanja vingi katika wilaya yake havina hati jambo alilolielezea kuwa wakati mwingine linawapa ugumu wa kuchukua hatua kwa wamiliki ambao baadhi yao wameyaacha kuwa mapori.

Kwa mujibu wa Mwaimu, wilaya hiyo imetoa miezi sita kwa wamiliki wote wa viwanja ambao hawajaviendeleza na kuviacha mapori vinginevyo watafutiwa umiliki wake.