Naibu Waziri ataka kufutwa mikataba kampuni urasimishaji

10Jan 2021
Munir Shemweta
Arusha
Nipashe Jumapili
Naibu Waziri ataka kufutwa mikataba kampuni urasimishaji

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, ameagiza kampuni za urasimishaji ambazo mikataba imekwisha na kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati, zinyang’anywe kazi hizo na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Sambamba na hilo, ameelekeza kampuni ambazo muda wa kazi bado haujaisha zifanye kazi chini ya uangalizi ili kuhakikisha zinakamilika kwa wakati.

Dk. Mabula alitoa agizo hilo jana mkoani hapa alipozungumza na watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa halmashauri akiwa katika ziara yake ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta hiyo na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi.Alisema kutokana na uamuzi huo, makatibu tawala wa wilaya katika mkoa wa Arusha, watumie mamlaka yao kuunda vikosi kazi kushirikisha halmashauri ili kuharakisha  urasimishaji kwenye maeneo ambayo kampuni za urasimishaji zimeshindwa kukamilisha kazi.

Awali, Dk. Mabula alisema baadhi ya kampuni za urasimishaji ardhi zimeshindwa kukamilisha kazi kwa wakati kwa visingizio mbalimbali na hata pale zilipokutana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, jijini Dar es Salaam.

Pamoja na kutoa visingizio hivyo, alisema ziliongezewa muda kukamilisha kazi lakini zilishindwa na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kazi hiyo.

"Kampuni ambazo mikataba yake imekwisha na kufikia Januari 31 hazijakamilisha kazi, zifungashe virago na kupelekwa katika vyombo vya sheria. Halmashauri zishirikiane na ofisi za ardhi za mkoa kufanya kazi hiyo," alisema Dk. Mabula.

Naibu Waziri Mabula alishangazwa na halmashauri kuweka malengo madogo katika ukusanyaji maduhuli ya serikali yatokanayo na kodi ya ardhi bila kujumuisha madeni ya wadaiwa sugu.

Alisema mkoa wa Arusha wenye wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi zaidi ya 200 una madeni ya zaidi ya Sh. bilioni 178.943, lakini mkoa ulijiwekea malengo ya kukusanya Sh. bilioni 8.9 tu na kukusanya Sh. bilioni 4.2 sawa na asilimia 47 hadi Desemba, mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo, aliwaelekeza maofisa ardhi wateule kuhakikisha wanawafikisha kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi kwa kuwa tayari walishapelekewa ilani za madai kama sheria inavyoelekeza.

Pia alisisitiza kuwa  wadaiwa wanaotaka majadiliano, wafanye hivyo ndani ya siku 14  na baada ya hapo, shauri lipelekwe kwenye baraza.

Baadhi ya wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi katika jiji la Arusha ni pamoja na taasisi mbalimbali za serikali zikiwamo Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambazo zimekubali kulipa madeni yao kwa awamu, huku Naibu Waziri akiagiza kuingia makubaliano kwa maandishi....kwa habari zaidi fuatilia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa