Naibu Waziri awajia juu maofisa misitu

26Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Naibu Waziri awajia juu maofisa misitu

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani, amewataka watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kubadilika katika utendaji wao na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kama walivyo zoea katika awamu za uongozi zilizo pita.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.

Makani aliyasema hayo juzi wakati alipokuwa akifungua warsha ya wadau wa mazao ya misitu nchini, iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, mjini hapa.

Alisema serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha inaleta mabadiliko katika kila sekta, hivyo kuwataka watumishi katika idara mbalimbali za misitu nchini, kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa hakuna atakayeendelea kuwalea.

“Watu wanashindwa kutofautisha kati ya uzoefu na mazoea hivyo basi wanajikuta wanafanyaka kama walivyozoea bila kuwaletea mabadiliko yoyote wananchi wanaowatumikia. Watumishi hao hawana nafasi katika serikali hii,” alisema.

Alisema Rais Dk. John Magufuli ameonyesha mfano katika utendaji wake wa kazi, hivyo watumishi hawana budi kufuata nyayo zake na kuachana na kufanya kazi kwa mazoea.

Kuhusu uvunaji wa mazao ya misitu nchini, Mhandisi Makani aliwataka wahusika kujipanga na kuhakikisha kazi hiyo inakuwa endelevu tofauti na ilivyo hivi sasa katika baadhi ya maeneo.

“Watu wanavuna misitu kwa wingi lakini hakuna jitihada za kuifanya misitu hiyo kuwa endelevu ili zao hili liendelea kuzalishwa kwa wingi na kuendelea kuliongezea pato taifa letu. Kama mnafanya hivyo mwisho wake mtavuna nini?” alihoji.

Alisema kila mwaka eka 372,000 za misitu huharibiwa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu kama vile kilimo , ufugaji na uchomaji mikaa.

Kwa upande wake. Ofisa Mtendaji Mkuu wa TFS, Juma Mgoo, alisema ili kukabiliana na uharibifu wa misitu, wameweka utaratibu wa kupanda eka 8,000 za miti kila mwaka.

Alisema mwaka jana walipanda eka 1,200 za miti katika maeneo mbalimbali lakini pia wamekuwa wakitoa elimu kwa wadau mbalimbali wa sekta ya misitu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali ndani ya sekta hiyo.

Habari Kubwa