Naibu Waziri Aweso amhenyesha mhandisi

13Jan 2019
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe Jumapili
Naibu Waziri Aweso amhenyesha mhandisi

NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amemwagiza Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Johannes Ngobya, kuwaomba radhi wananchi wa vijiji vya Kyamulaile na Mashule.

NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, picha mtandao

Mhandisi huyo alipewa maagizo hayo baada ya kudaiwa kusema uongo kuwa mradi wa uchimbaji visima vya maji katika vijiji hivyo unaendelea.
 
Akizungumza katika eneo la mradi, Aweso alisema mhadisi huyo alidanganya katika taarifa yake kuwa mkandarasi ameshaweka vifaa katika eneo la mradi na kwamba mradi huo unaendelea.
 
"Wananchi wa vijiji hivi waliathiriwa na tetemeko la ardhi, nadhani ndiyo wangepewa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi kwa kuwatatulia tatizo hili kwa dharura, lakini hakuna kinachofanyika, mnaendelea kuwatesa," alisema.

Alisema katika taarifa yake Mhandisi huyo alisema zimetengwa Sh. milioni 85 ikiwa ni sehemu ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/2019  kwa ajili ya kuweka vifaa katika eneo la mradi na kuanza uchimbaji wa visima, lakini hakuna kinachofanyika.
 
"Kawaombe radhi wananchi wa Kyamulaile na Mashule, kwa nini unasema uongo na kuendelea kuwatesa. Hapa kuna kifaa chochote kweli? Mimi nimetoka Dodoma nimefika hapa nikaona hakuna kifaa chochote. Wewe uko hapa hapa ofisini lakini hufahamu chochote kinachoendelea?" alihoji.
 
Alisema kama mhandisi huyo amesema uongo mbele ya Naibu Waziri, basi hakuna mradi anaoweza kutekeleza na kuwa wahandisi wa aina hiyo hawatakwenda nao katika kipindi ambacho wanataka kuanzisha wakala wa maji vijijini.
 
"Tunahitaji kwenda na wahandisi wenye uwezo wa kufanya kazi kwa kusimamia miradi ipasavyo, wenye weledi na waadilifu," alisema.
 
Akiomba radhi kwa wananchi hao, mhandisi huyo alidai kuwa kwa mujibu wa mkataba alidhani mkandarasi tayari yuko eneo la mradi, kauli ambayo ilikemewa vikali na Naibu Waziri.
 
“Inakuwaje unakaa ofisini tu hutoki kujiridhisha, ndiyo maana unaandika taarifa za uongo kama hizi," alisema.
 
Awali, akipokea taarifa na kuzungumza na baadhi ya watumishi katika Manispaa ya Bukoba, Naibu Waziri huyo alisema watafanya mchujo wa wahandisi ambao watafaa kusimamia miradi kupitia wakala na kuwa hawako tayari  kuwatumia wahandisi wababaishaji.

 

Habari Kubwa