Naliandalia taifa wasomi wasio na mashaka- Msekwa

07Dec 2019
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Naliandalia taifa wasomi wasio na mashaka- Msekwa

SPIKA wa zamani wa Bunge la Tanzania, Pius Msekwa, amesema kati ya wasomi 1,773 wanaotokana na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), wamo nguli wa kitaaluma walioandaliwa kulisaidia taifa kuja na matokeo chanya ya tafiti mbalimbali.

Alisema kundi hilo la wasomi linaloingia katika soko la ajira ni kwa ajili ya matumizi ya jamii ili kujenga uchumi na kupunguza umasikini.

Msekwa aliyasema hayo jana mjini Moshi, wakati wa mahafali ya tano ya chuo hicho.

"Chuo hiki ni miongoni mwa vyuo vikuu vya umma vilivyo chini ya Wizara ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, tumepewa jukumu zito la kuandaa wataalam wa fani mbalimbali wakati huu taifa likielekea katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

"Katika kipindi cha mwaka wa masomo 2018/2019 tumefanikiwa kulisaidia taifa kuzalisha wataalam hao 1,773.

Tujipange zaidi kutekeleza majukumu yetu kama kutoa huduma za ushauri unaohusiana na maendeleo ya ushirika na biashara kwa wadau wa ushirika, asasi za biashara na watu binafsi."

Wasomi hao wanatoka katika kitivo cha ushirika na maendeleo ya jamii (FCCD), kitivo cha biashara na sayansi za mawasiliano (FBIS), kurugenzi ya maktaba ya ushirika na nyaraka za kale (DLS) na taasisi ya elimu endelevu ya ushirika (ICCE).

Msekwa kwa sasa, ndiye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Awali, Makamu mkuu wa chuo hicho Prof. Alfred Sife kati ya wanataluma hao waliohitimu mafunzo ya muda mrefu limo kundi la wahitimu katika programu za shahada ya umahiri ya Ushirika na maendeleo ya jamii (MA-CCD), shahada ya umahiri ya menejimenti ya manunuzi na ugavi (BA-PSM) na shahada ya umahiri ya menejimenti ya biashara (MBM).