Nanasi husaidia kudhibiti kiharusi ‘presha’,

31Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Nanasi husaidia kudhibiti kiharusi ‘presha’,

LICHA ya kwamba nanasi ni miongoni mwa matunda matamu ya msimu ambayo kwa hapa nchini hupatikana kwa wingi miezi ya mwishoni mwa mwaka, -

Iimefahamika kuwa  lina faida nyingi kwa walaji, ikiwamo kuwapunguzia uwezekano wa kupata baadhi ya maradhi ya kansa, shinikizo la damu maarufu ‘presha’ na kiharusi.

 

Kwa mujibu wa majarida mbalimbali ya afya na lishe yatokanayo na ripoti za utafiti, inaelezwa kuwa nanasi limejaliwa wingi wa viinilishe vyenye manufaa makubwa kwa walaji.

Katika andiko lililomo kwenye mtandao wa ‘organicfacts’ ambao huchambua kisayansi masuala mbalimbali ya tiba na lishe, inaelezwa kuwa baadhi ya viinilishe vilivyomo kwenye nanasi ni vya jamii ya vitamin na madini; miongoni mwao ni potassium, shaba, manganese, calcium, vitamin C, beta-carotene, thiamin, vitamin B6, folate, nyuzinyuzi za kuyeyuka na zisizoyeyuka na pia bromelain.

“Viinilishe hivyo vilivyomo kwenye nanasi, ndivyo vinavyolipa tunda hilo uwezo wa kuukinga mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali yakiwamo ya shinikizo la damu na  saratani,” inaelezwa na daktari mmoja wa masuala ya lishe aliyezungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki.

Aidha, inaelezwa kuwa mbali na kuupatia mwili wa mlaji kiwango kizuri cha maji, nanasi pia huimarisha mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa na hivyo kuwaweka salama walaji dhidi ya matatizo mbalimbali ya kiafya yakiwamo ya mifupa.

Faida nyingine wanazopata walaji wa mananasi ni kuwapunguzia walaji uwezekano wa kupata matatizo ya upumuaji, mmeng’enyo wa chakula, kifua na mafua na pia uzito wa mwili uliopitiliza.

Kadhalika, kwa mujibu wa ripoti kuhusu nanasi, inaelezwa kuwa viinilishe vya tunda hilo husaidia pia kuponyesha haraka vidonda na majeraha, kuimarisha afya ya kinywa, kuongeza uoni, kudhibiti shinikizo la damu (presha), maradhi ya moyo, kiharusi na pia kuimarisha mzunguko wa damu katika kiwango kinachohitajika mwilini.

 

KUZUIA KANSA, PRESHA, KIHARUSI

Nanasi huhusishwa moja kwa moja na uwezo wa kuzuia baadhi ya kansa (saratani) mwilini mwa walaji zikiwamo za mdomo, koo na matiti kutokana na kujawa na kiwango cha juu cha viinilishe vya kinga (antioxidants) vikiwamo vitamin A, beta carotene, manganese, bromelain na kampaundi za ‘flavonoid’.

Aidha, inaleezwa vilevile kuwa nanasi husaidia kudhibiti shinikizo la damu mwilini mwa walaji kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha madini yakiwamo yapotassium, ambayo ndiyo huhusika moja kwa moja katika kukabili shinikizo la juu au la chini kwenye mishipa ya damu. Pia potassium husaidia mwili kufikisha damu kwa usahihi kwenye maeneo yote na hivyo kuufanya uwe salama zaidi kwa kuwa na kiwango sahihi cha damu katika kila kiungo.

Kwa sababu hiyo, faida zaidi za madini hayo yaliyomo kwenye nanasi kama potassium ni kuuweka mwili mbali na uwezekano wa kupatwa na matatizo ya kuwapo mabonge kwenye mfumo wa damu na kusababisha maradhi ya moyo na kiharusi,

ULAJI WAKE

Inaelezwa kuwa zipo njia nyingi za ulaji nanasi kwa usahihi na mojawapo ni kulila likiwa ‘fresh’ baada ya kuiva na kuvunwa; kunywa juisi yake, kwa kulipika na pia kula lililohifadhiwa vyema bila ya kupotezewa viinilishe vyake.

 

*Imeandikwa kwa msaada wa mtandao (www.organicfacts.net)