Nape azidi kuitetea Sheria ya Huduma Vyombo vya Habari

09Dec 2016
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Nape azidi kuitetea Sheria ya Huduma Vyombo vya Habari

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema hakuna upungufu uliopo katika Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari utaoshindwa kutatulika endapo kutakuwa na nia ya dhati kati ya serikali na wadau wenyewe kukaa meza moja na kuzungumza.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Nape alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa wadau wa vyombo vya habari kujadili namna ya kuendana na sheria hiyo mpya.

Pia alisema anamini sheria hiyo siyo mbaya kama ilivyokuwa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.

Kwa mujibu wa Nape, sheria hiyo ya magazeti ya mwaka 1976, imempa mamlaka makubwa waziri mwenye dhamana.

Hata hivyo, alisema sheria ya sasa imeondoa mamlaka makubwa aliyokuwa nayo.

Alisema anafahamu ipo hofu kwa wadau wa habari juu ya sheria hiyo, lakini ni vema wakaondoa hofu hiyo kwa sababu anaamini hakuna jambo litakaloshindikana kadiri watakavyoendelea kuisoma, kuijadili na kuzungumza.

Alisema ikumbukwe kwamba mchakato wa maandalizi ya sheria hiyo umechukua zaidi ya miaka 20 na imetungwa na binadamu, hivyo haiwezi kuwa kamilifu kwa asilimia 100 na kukidhi haja za watu wote japokuwa anaamini imekidhi kiu ya watu wengi.

“Kumekuwa na hofu kubwa ambayo imejengwa kwa wanahabari kuhusiana na sheria hii mpya, sioni sababu ya kuendelea kujenga hofu hiyo japokuwa si vema kuondoa hofu yote ili msibweteke iwasaidie kutekeleza majukumu yenu vizuri. Kwenye sheria hii ukiangalia historia nzima ya mchakato wake ulijenga mazingira ya kutoaminiana kati ya wadau wenyewe,” alisema Nape.

Alisema yapo baadhi ya mambo kwenye sheria hiyo ambayo kwa sababu ya namna yalivyokwenda kwenye mijadala, waliona kuna umuhimu wa kuyaweka kwenye kanuni kwa sababu kwanza mjadala wake haukufikia mwisho, lakini pia kubadilisha kanuni ni rahisi kuliko kubadilisha sheria.

“Kwa hiyo tukiona kuna maeneo yana tatizo, tutarudi mezani tutayarekebisha na tukasonga mbele,” alisema.

Alisema sheria imetoa mamlaka ya kila kitakachobadilishwa katika kanuni za sheria hiyo kutekelezwa ndani ya miaka mitano na kwamba katika kipindi cha miaka hiyo, kuna umuhimu kwa wadau kuhakikisha wanaboresha maeneo muhimu ambayo yatasaidia kuboresha tasnia hiyo.

“Kadiri wadau wanavyoendelea kuipitia na kuijadili sheria hii, nina matumani na inawezekana yakawapo maeneo yenye upungufu ambao naamini siyo ya kuua tasnia, yanayoweza kuzungumzwa na yakajadiliwa," alisema.

Katibu Mkuu wa TEF, Neville Meena, alisema changamoto kubwa inayowaumiza kichwa wadau wa habari si aina ya wanahabari wanaokwenda kufanya kazi katika vyombo hivyo, isipokuwa ni kutokuwapo kwa mfumo bora wa elimu katika sekta nzima ya elimu ambao unaweza kutoa wanataaluma bora bila kujali ni wanahabari ama taaluma nyingine.

“Hatukatai mwandishi wa habari kuwa na elimu, lakini ‘pressure’ iliyopo katika vyumba vya habari ni kwamba ni mfumo upi utakaowaandaa waandishi wa habari na kuja katika vyombo vya habari wakiwa wameiva, na hii si kwa wanahabari tu pia na taaluma nyinginezo, mfumo uliopo haumwandai mwanataluuma kuwa zao bora katika sekta ya ajira. Tunaomba serikali iliangalie na hili,” alisema Meena.

Pia alisema lipo tatizo lingine kwa maofisa wa serikali wanaoshughulikia katika idara za habari kutokuwa na uwezo wa kutosha wa kujieleza katika vyombo vya habari na hivyo kuchangia serikali kuandikwa vibaya ama taarifa zake kutopatikana.

Mwenyekiti mstaafu wa TEF, Absalom Kibanda, alisema hofu katika sheria hiyo haipo kwa wana habari isipokuwa kwa serikali na kwamba ndiyo kulikuwa na mvutano mkubwa katika kuipitisha sheria hiyo.

“Miaka 10 tumeishi katika giza, tumeingia katika miaka mitano mingine ya hatari, si kwa mawaziri kwa viongozi hata kwa wanahabari,” alisema Kibanda.

Habari Kubwa