Nape: Bil.283/- kuleta mapinduzi ya kiuchumi

21May 2022
Romana Mallya
DODOMA
Nipashe
Nape: Bil.283/- kuleta mapinduzi ya kiuchumi

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema bajeti ya wizara hiyo ya Sh. bilioni 282.5 katika mwaka wa fedha 2022/23, imelenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi kupitia utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Akiwasilisha jana bungeni jijini Dodoma makadirio ya mapato ya matumizi ya wizara hiyo, Waziri Nape alisema mradi huo unalenga kuleta mabadiliko ya kidijitali kwa kuwezesha maunganisho ya kijiditali ya kikanda na kimataifa ili kukuza uchumi katika eneo hilo.

Alisema wizara yake inasimamia mapinduzi hayo na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

"Mapinduzi ya kidijitali ndiyo yanayoweka msingi wa kulipeleka Taifa kwenye uchumi wa kidijitali unaowezeshwa na kuendeshwa na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,” alisema.

Alisema wizara imepanga kufanya mabadiliko na maboresho kwenye sekta ili kuendana na mageuzi kwa kuharakisha uendelezaji na usimamiaji miundombinu ya TEHAMA, mawasiliano, posta na habari anwani za makazi, mitambo ya utangazaji na posta.

Nape alisema mapinduzi hayo yanawezeshwa na misingi muhimu ikiwamo TEHAMA, mifumo ya mawasiliano, tendaji, fedha, usambazaji kwa njia ya posta, uwapo wa vyombo vya upashanaji habari pamoja na uimara wa uhuru husika.

Aidha, alisema uchumi wa kidigitali unawekewa mazingira bora ya kiudhibiti, kiuwekezaji na matumizi kwa ajili ya uanzishwaji na uendelezaji wa kampuni changa.

Alisema matokeo ya mradi huo ni pamoja na kuongeza na kubuni ajira zitakazotokana na ubunifu wa TEHAMA, ukuzaji wa viwanda vidogo na kukuza ustadi wa wataalamu wa ndani ya serikali na waliopo nje ya Serikali.

Matokeo mengine ni kuongeza uwezo wa utoaji wa huduma za serikali kwa kuwezesha uwapo wa intaneti bora ya bei nafuu na ya uhakika kwa ajili ya matumizi ya serikali ili kumnufaisha mwananchi.

Nape alisema katika mwaka 2022/23, Wizara inakadiria kutumia kiasi cha Sh. bilioni 39.3 ikiwa ni fedha za nje kwa ajili ya kujenga kituo kimoja cha kukuza taaluma na ubunifu katika TEHAMA na vituo vidogo vitano kwenye kila Kanda.

Alisema fedha hizo zitawezesha ununuzi, ugavi na ufungaji wa vifaa katika kituo kimoja kikubwa na vituo vidogo vitano vya kukuza taaluma na ubunifu katika TEHAMA na kuwezesha ununuzi wa ‘bandwidth’ kwa ajili ya matumizi ya intaneti ya serikali.

Alisema pia watafanya mapitio na kuhuisha sera, sheria na kanuni mbalimbali za TEHAMA, kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA nchini kwa kuwapatia wataalamu 200 mafunzo ya muda mfupi na wataalamu 10 mafunzo ya muda mrefu na kufanya tathmini ya kuainisha mahitaji na usanifu wa kujenga mfumo wa kuwezesha biashara mtandao.

ANWANI ZA MAKAZI

Kuhusu anwani za makazi, Nape alisema hadi Aprili mwaka huu jumla ya anwani za makazi 12,171,320 zimekusanywa na kuingizwa kwenye programu tumizi.

MKONGO WA TAIFA

Alisema hadi Aprili mwaka huu wamekamilisha taratibu za manunuzi za kuwezesha ujenzi wa kilomita 4,442 kutoka kiwango cha 200G hadi 800G na kujenga vituo 37, upanuzi wa vituo 75 vya kutoa huduma ambavyo mikataba 22 ya Sh. bilioni 141 imesainiwa.

Habari Kubwa