Nassari akaribishwa kujiunga CCM

29May 2019
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Nassari akaribishwa kujiunga CCM

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM), Raymond Mwangwala, amemkaribisha aliyekuwa Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joshua Nassari kuingia katika chama hicho.

Aliyekuwa Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joshua Nassari.

Ukaribisho huo aliutoa jana katika Kijiji cha Mbuguni, wilayani Arumeru wakati alipokuwa akitoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu na jamaa wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Thomas Mollel, maarufu kwa jina la Askofu.

Alisema Nassari ni kijana mwenye uwezo mkubwa wa kifikra na hivyo anaamini katika hatua ya sasa atafanya maamuzi yalio sahihi kwa kuwa ni kijana.

"Mimi nawapa pole kwa msiba huu na nipo msibani hapa kumzika Askofu Thomas, lakini nitumie fursa hii pia kumkaribisha Nassari kuja CCM na mimi nitampokea maana nipo hapa Arusha," alisema.

Aidha, alimpongeza Mbunge mpya Dk. John Pallangyo, aliyeapishwa hivi karibuni bungeni Dodoma na kumtaka kufanya kazi za kuwaletea maendeleo wananchi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Loata Sanare, alimtaka mbunge mpya kutekeleza mipango ya Askofu Thomas kwa kuwasaidia wahitaji wa jimbo hilo.

Alisema muda wa kupambana kisiasa umeisha na kiongozi amepatikana kilichobaki wote kushirikiana kuwaletea wananchi maendeleo.

"Tena nampongeza Nassari kwa kuja katika msiba wa kada wetu CCM na huo ndio uungwana tuliouzoea Tanzania hivyo sio mbaya nawe ukimuunga mkono marehemu Askofu Thomas kwa kujiunga CCM," alisema.

Sanare alisema marehemu alifanya mambo mengi mazuri ambayo vema kila kiongozi akamuenzi kwa kutekeleza ikiwamo kujali wahitaji kama yeye alivyotumia utajiri wake kusaidia wahitaji mbalimbali na kujenga shule na vituo vya afya.

Habari Kubwa