Nauli mpya za mabasi yote kuanza kutumika leo

08Dec 2023
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Nauli mpya za mabasi yote kuanza kutumika leo

NAULI mpya za mabasi ya mjini(daladala) na za mabasi ya masafa marefu zimeanza kutumika leo.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), hakuna pingamizi lolote walilopokea kutoka kwa wadau tangu watangaze nauli hiyo.

LATRA kupitia bodi yake, ilitangaza ongezeko hilo la nauli baada ya kupitia maoni ya wadau na kutoa siku 14 kwa watu kuwasilisha pingamizi kuhusu nauli hizo mpya.

Kwa mujibu wa LATRA, umbali usiozidi kilomita 10 ambayo awali nauli yake ilikuwa ni Sh.500, nauli ya sasa ni Sh.600,  wakati kwa kilomita 11 hadi 15 iliyokuwa Sh.550 kwa sasa ni Sh.700

Kadhalika, kwa umbali wa kuanzia kilomita 16 hadi 20 ambayo awali ilikuwa Sh. 600 kwa sasa ni  Sh.800 wakati kuanzia kilomita 21 hadi 25 iliyokuwa ikitozwa Sh.700 kwa sasa ni Sh.900.

Pia, umbali wa kuanzia kilomita 26 hadi 30 ambayo nauli yake awali ilikuwa Sh.850, ya sasa ni Sh.1,100 wakati kwa kilomita 31 hadi 35 ambayo ilikuwa Sh.1,000, ya sasa ni Sh.1,300.

Kilomita 36 hadi 40 ambayo nauli yake ilikuwa Sh.1,100  kwa sasa ni Sh.1,400.

Kwa mabasi ya masafa marefu, basi la kawaida kwenye barabara ya lami ambayo nauli yake ilikuwa Sh.41.29 kwa kilomita, kwa sasa ni Sh.48.47 kwa kilomita,  wakati basi la aina hiyo kwa barabara ya vumbi ambayo awali nauli yake ilikuwa Sh.51.61,kwa kilomita, kwa sasa ni Sh.53.32.

Basi la kati ambalo nauli yake ilikuwa inatozwa kwa Sh.56.88 kwa kilomita kwa barabara ya lami,  kwa sasa ni Sh.67.84.