NBC yatoa bil.2/- kukopesha wastaafu

19Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
NBC yatoa bil.2/- kukopesha wastaafu

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa mikopo yenye jumla ya kiasi cha Sh.bilioni 2.1 kwa wastaafu tokea ilipozindua huduma ya mikopo ya wastaafu Juni mwaka jana.

 

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Theobald Sabi, Mkurugenzi wa Wateja Binafsi, Gaudence Shawa, katika uzinduzi rasmi wa Tawi jipya la Benki hiyo la Tegeta Kibo Commercial Complex, alisema benki hiyo imewatambua wastaafu kama kundi muhimu la kiuchumi.

“NBC tumewatambua wastaafu wanaopokea pensheni kama kundi la kiuchumi ambalo lina uwezo wa kuchangia katika uchumi wa taifa letu kwa kuwezeshwa kifedha,” alisema.

“Kikwazo kikubwa, kwa siku za huko nyuma, ilikuwa kutokuwapo kwa bima ya mikopo kwa watu waliovuka umri wa miaka 60, sasa ipo bima inayowakinga wastaafu waliovuka umri huo nchini,” aliongeza Sabi.

Alifafanua kwamba kwa kutambua umuhimu wa wafanyabiashara wadogo na wa kati, mwaka 2016, uongozi wa benki hiyo waliunda kurugenzi maalum ya kuhudumia wateja hao na hadi Machi mwaka huu benki hiyo imeshatoa jumla Sh. bilioni 155 kama mikopo kwa wafanyabiashara 3,000 nchini.

Aliongeza kwamba benki hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) ambalo ni Benki tanzu ya Benki ya Dunia imefanya mapitio ya kina ya utaratibu mzima wa utoaji wa mikopo katika kundi hilo ili kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa viwanda nchini.

Shawa alifafanua kwamba benki hiyo imewawezesha wateja binafsi takribani 27,000 kwa mikopo isiyokuwa na dhamana yenye thamani Sh. 337,000 kati ya hao asilimia 53 ni watumishi wa serikali na asilimia 47 ni kutoka sekta binafsi.

“Azma ya benki hii ni kuwakuza wafanyabiashara wadogo hadi wafikie hatua ya kuchangia katika uchumi wa Tanzania na katika kutimiza lengo hilo benki hii imezindua klabu za biashara zijulikanazo kama ‘Business Clubs” katika mikoa mbali mbali nchini,” alisema.

Alisema dhumuni la kuanzisha klabu hizo ni kuwajengea uwezo wafanyabiashara hao kwa mafunzo maalum ya kuendesha biashara zao kwa njia ya kisasa na kuongeza uzalishaji, faida na tija ya uendeshaji.

Shawa aliongeza kwamba mafunzo hayo yanaratibiwa na benki hiyo kwa kushirikiana na taasisi kadhaa kama vile Mamlaka ya Biashara Tanzania, Kituo cha Uwekezaji (TIC), Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO), Chama cha wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Pamoja na mambo mengine, hadi kufikia Disemba mwaka jana, benki hiyo ilikuwa imetoa mafunzo hayo kwa takribani wafanyabiashara 7,000 na lengo ni kuwafikia zaidi ya 1,000.

Habari Kubwa