NBC yawafunda wastaafu watarajiwa Morogoro, Mtwara na Zanzibar

05Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
NBC yawafunda wastaafu watarajiwa Morogoro, Mtwara na Zanzibar

WATUMISHI wanaotarajiwa kustaafu katika taasisi za serikali na mashirika binafsi, wametakiwa kuweka mikakati thabiti ya matumizi bora ya fedha sambamba na kupata elimu sahihi kuhusu huduma za kifedha na uwekezaji wa miradi sahihi ili wafaidike na mafao yao baada ya kukoma utumishi.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (Katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa wakati wa semina ya Watumishi wanaotarajiwa kustaafu katika taasisi za serikali na mashirika binafsi iliyoandaliwa na mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) jijini Dar es Salaam na kudhaminiwa na wadau mbalimbali ikiwemo benki ya NBC.

Viongozi waandamizi wa NBC katika mikoa ya Morogoro, Mtwara na Zanzibar walisema hayo walipopata fursa ya kuzungumza na wastaafu hao watarajiwa kwenye semina ya siku mbili iliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na kudhaminiwa na wadau mbalimbali ikiwamo benki hiyo.

Akizungumza kwenye moja ya semina hizo mkoani Morogoro, Meneja Mikopo wa  NBC, Mtenya Cheya, aliwataka watumishi hao kuheshimu na kutunza fedha katika taasisi zinazoaminika sambamba na kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato kwa kufuata ushauri madhubuti kutoka kwa wataalamu.

Tunawapenda! Meneja Mikopo NBC, Makao Makuu Mtenya Cheya akizungumza na wastaafu watarajiwa wakati wa semina ya watumishi wanaotarajiwa kustaafu katika taasisi za serikali na mashirika binafsi iliyoandaliwa na mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) jijini Dar es Salaam na kudhaminiwa na wadau mbalimbali ikiwemo benki hiyo.

“NBC tumejipanga kuwasaidia wastaafu watarajiwa na wale waliokwishastaafu ndiyo maana pamoja na kushiriki kwenye semina za mafunzo kama hizi, pia tumekuwa na mikakati na huduma bora kwa wastaafu ikiwamo kutoa mikopo inayozingatia mahitaji yao,’’ alisema.

Katika semina kama hiyo iliyofanyika mkoani Mtwara, Meneja wa NBC Tawi la Mtwara, Emmanuel Mseti, aliwataka wastaafu hao watarajiwa kuhakikisha wanawashirikisha wataalamu wa fedha pindi wanapofikiria kuhusu mawazo ya biashara, uwekezaji na matumizi sahihi ya mikopo ili kujihakikishia ufanisi wa matumizi ya mafao yao.

“Ndio maana Benki ya NBC tumekuwa na utaratibu mzuri wa kuwapatia mafunzo wateja wetu kupitia mipango mbalimbali ukiwamo mpango wa klabu za biashara na utoaji wa mafunzo ya ujasiriamali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Lengo ni kuwajengea uwezo kufanya biashara kabla hatujawakopesha,’’ alisema.

Wito kama huo pia ulitolewa Zanzibar na Mkuu wa Bidhaa na Mauzo wa Benki hiyo, Abel Kaseko, aliyewasihi wastaafu hao watarajiwa kuhakikisha wanahifadhi pesa zao kwenye taasisi rasmi za kifedha ili kuepuka matapeli.

Baadhi ya maofisa wa benki ya NBC tawi la Morogoro wakiongozwa na Meneja wa tawi hilo Sophia Mwombela (Kulia) wakifuatilia semina ya Watumishi wanaotarajiwa kustaafu katika taasisi za serikali na mashirika binafsi iliyoandaliwa na mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na kudhaminiwa na wadau mbalimbali ikiwemo benki hiyo. Wengine ni Meneja biashara NBC Morogoro, Joseph Boaz (Kushoto) na Meneja mikopo NBC makao makuu Mtenya Cheya (Katikati).

“Zaidi pia tuhakikishe tunaanza uwekezaji mapema ili kujijengea uzoefu utakaotusaidia kujiandaa na maisha ya baadaye. Ifahamike kwamba matumizi sahihi ya fedha hizi ndiyo yatakayosaidia wengi wetu kuondokana na utegemezi baada ya kustaafu,’’ alisema.

Pamoja na kuishukuru benki hiyo kwa nasaha hizo muhimu, washiriki wa mafunzo hayo kutoka katika taasisi mbalimbali walielezea namna walivyonufaika na mafunzo hayo.

Pia walikiri kwamba wengi wao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kushindwa kujiwekea akiba, matumizi yasiyo sahihi ya mafao baada ya kustaafu na kushindwa kubuni mawazo mazuri ya uwekezaji wa fedha hizo.

“Niwashukuru sana watu wa PSSSF kwa kuhusisha wataalamu mbalimbali kwenye semina hizi zikiwamo benki kama NBC kwa kuwa wametufumbua macho kwenye mambo mengi. Kwa kweli kupitia elimu hiyo itatusaidia sana,’’ alisema Ali Mselem Ali, mstaafu mtarajiwa kutoka Zanzibar.

Semina hiyo ilipambwa na uwepo wa viongozi waandamizi wa serikali katika mikoa hiyo wakiwamo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigela, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti.