NCCR yaanika vipaumbele 10

06Sep 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
NCCR yaanika vipaumbele 10

CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimezindua kampeni zake za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kikiainisha vipaumbele vyake 10 kama kitachaguliwa kushika dola, ikiwamo kuzingatia utu na usawa wa kijinsia.

Tukio hilo lililoambatana na uzinduzi wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho iliyopewa jina la ‘Mwafaka wa Kitaifa’, lilifanyika kwenye Viwanja vya Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam jana.

Katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Elizabeth Mhagama, alisema ilani imefanyiwa utafiti na imejibu matatizo mengi yanayoikabili nchi.

“Ni Ilani ambayo inalileta taifa letu kuwa moja, imetokana kwa kuangalia rasimu ya Jaji Warioba, na imefanyiwa utafiti. Nia ya kuandika katiba mpya tunayo na uwezo tunao,” alisema Mhagama.

Vipaumbele vya chama hicho ni pamoja na kuufufua mchakato huo wa katiba mpya na kuboresha sekta ya elimu kwa kuwa na falsafa ya elimu ifaayo kwa nchi.

Vingine ni mwafaka wa kitaifa utakaohusu maridhiano juu ya maadili ya kitaifa, kuimarisha na kuboresha afya na ustawi wa jamii, kuboresha mazingira na makazi kwa wananchi, ustawi wa vyombo vya habari na asasi zisizo za kiserikali na kuimarisha usawa wa kijinsia kwa kuhakikisha kunakuwa na idadi sawa ya wanaume na wanawake katika vyombo vya uwakilishi.

Kwa mujibu wa ilani hiyo, vipaumbele vingine vya chama hicho ni kuimarisha uchumi, ulinzi na usalama na kupiga vita dhidi ya rushwa kwa kutengeneza vyombo vyenye nguvu kubwa na mtandao mkubwa wa kuvidhibiti.

Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, alisema wameweka misingi ya mwafaka wa kitaifa kwa sababu kumeanza kuonyesha dalili za baadhi ya watu kujionyesha wao ni bora kuliko wengine.

Mbatia alisema anakumbuka wosia ulioachwa na aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, wa kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu unakuwa huru na haki.

“Mzee huyu alituachia wosia mzuri wa kuifanya Tanzania inakuwa sehemu nzuri ya kuishi, tuheshimu wosia huu wa mzee aliotuachia,” alisema.

Mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho, Yeremia Maganja, alisema akiingia madarakani, atawaita Rais John Mafufuli, Bernard Membe, Profesa Ibrahim Lipumba, Tundu Lissu na Maalim Seif Sharif Hamad katika meza ya maridhiano ya kitaifa.

Maganja pia alisema akiingia madarakani, ndani ya miezi 12 hadi 18, atakuwa amewapatia Watanzania katiba mpya.

Habari Kubwa