NCCR yaipa serikali mbinu kukabili corona

03Dec 2021
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
NCCR yaipa serikali mbinu kukabili corona

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimeishauri serikali kuwa na meza ya mazungumzo na wadau kupata mbinu mpya za kukabiliana na matatizo mbalimbali yanayolikabili taifa ikiwamo ugonjwa wa UVIKO-19.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema taifa limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo hadi sasa hazijapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Alishauri kuwa nchi ionyeshe ushirikiano na siyo ushindani katika suala la kinga, utayari na mwitikio katika kupambana na janga hilo ili kuweza kulikabili kwa maslahi ya kulinda afya za Watanzania.

“Duniani leo tatizo hili la virusi vinavyosababisha ugonjwa wa UVIKO-19 kuna hiki kilichogundulika kama wiki mbili zilizopita, jana, juzi Shirika la Afya Duniani (WHO), lilisema kama dunia ilishindwa kupambana na kirusi aina ya Delta, je, hiki kipya tutakiweza hiyo ni lugha ya dunia.

Aliwashauri viongozi kuwa wawe mstari wa mbele na mfano wa kuigwa katika kupambana na tatizo hilo.

Kwa mujibu wa Mbatia, dunia iko mbioni kuja na mkataba wa kidunia katika kulinda afya za watu dhidi ya janga hilo huku akiwaasa viongozi kuwa waache kuongea wanavyojua bali wakubali kufuata ushauri wa wataalamu.


Alisema NCCR-Mageuzi inaomba ushirikiano wa Watanzania na dunia katika kupambana na jambo hilo kwa kuwa na utayari, na alitoa wito kwa wasiopata kinga waweze kuchanja ili kulinda afya zao.

“Kuna viongozi wengine wanasimama kwenye majukwaa wanazungumzia UVIKO-19, lakini wenyewe hawajachanja. Mimi binafsi ninajiamini kuzungumzia hili kwa kuwa nilichanja hadharani na familia yangu na viongozi wote wakuu wa chama, kuonyesha kuwa kiongozi ni kuwa kielelezo,” alisema Mbatia.

Pia alishauri kuwa nchini kila baada ya wiki kutolewe takwimu zinazoonyesha ni watu wangapi wamechanjwa.
 

Habari Kubwa