Nchi 15 kuleta waangalizi wa uchaguzi

16Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Nchi 15 kuleta waangalizi wa uchaguzi

SERIKALI imeziruhusu nchi 15 kupitia balozi zao nchini zimeruhusiwa kuleta waangalizi wa kimataifa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, 2020.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi na kwamba hatua hiyo imechukuliwa baada ya balozi hizo kuwasilisha maombi na kufuata taratibu.

Prof. Kabudi aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU), Balozi Manfred Fanti na kuongeza kuwa uchaguzi wa mwaka huu kwa mara ya kwanza umekuwa tofauti na miaka iliyopita, kwa kuwa unafanyika kwa kugharamiwa na fedha za ndani badala ya wahisani jambo ambalo baadhi ya watu walianza kuhofia kutokuwapo kwa waangalizi wa kimataifa.

"Huu ni uchaguzi mkuu ambao kwa mara ya kwanza kwa asilimia 100 tunaugharamia sisi wenyewe kama Serikali ya Tanzania, utaratibu wa uchaguzi chini ya sheria ya uchaguzi na chini ya utaratibu wa kimataifa huwa tunakuwa na waangalizi wa uchaguzi na mwaka huu nchi hizo 15 kupitia balozi zao zimepata kibali baada ya kufuata taratibu za kuomba kuleta waangalizi wa uchaguzi mkuu," alisema Prof. Kabudi.

Mbali na huyo wa EU, pia Prof. Kabudi alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini, Balozi Roberto Mengoni na baadaye Balozi wa Poland, Balozi Krzysztof Buzalski ambapo amewakabidhi vitabu vya sheria ya uchaguzi na kanuni za uchaguzi na miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya uchaguzi ili kuwapa fursa ya kufahamu namna uchaguzi unavyoendeshwa nchini hususani baada ya uwapo wa malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani juu ya kuenguliwa kwa wagombea wao.

Kwa upande wake Balozi Fanti alisema Nchi za Umoja huo zimekuwa zikifuatilia kwa karibu mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu zinavyoendelea nchini ambapo mpaka sasa wanaridhishwa na kampeni zinavyofanyika kwa uhuru na amani na sasa wanajiandaa na zoezi la uangalizi wa uchaguzi huo.

Balozi wa Italia nchini Roberto Mengoni, alisema amevutiwa na namna vyombo vya habari vimekuwa vikitoa nafasi kwa wagombea wote kwa uhuru na bila ya ubaguzi na kupongeza namna Watanzania wanavyojitokeza kwa wingi kusikiliza sera za wagombea mbali na tishio la corona, na kwamba ana imani kuwa kiongozi atakayechaguliwa atakuwa ametokana na utashi wa wananchi.

Mbali na masuala ya uchaguzi mkuu, Waziri Kabudi na Mabalozi hao walijadili pia masuala ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, maendeleo ya kiuchumi, biashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu, afya, maji na miundombinu.

Habari Kubwa