Ndalichako aipa rungu Nacte kufungia vyuo

10Aug 2018
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ndalichako aipa rungu Nacte kufungia vyuo

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amelitaka Baraza la Uongozi la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), kuvifungia vyuo vyote vya umma na binafsi ambavyo havijakidhi vigezo na matakwa ya serikali yaliyowekwa katika sekta ya elimu.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

Profesa Ndalichako alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizindua baraza hilo na kusema kuwa serikali haitaki kuwa na utitiri wa vyuo ambavyo vinawapotezea muda wa Watanzania.

Alisema vyuo ambavyo havijakidhi vigezo vifungwe mara moja ili kuwa na vichache vyenye ubora na ujuzi unaotakiwa kisheria.

“Hatuwezi kuviacha vyuo vitoe mafunzo kiholela ni muhimu baraza kuhakikisha linasimamia na kuwaongoza wamiliki wanaohitaji kuanzisha vyuo hapa nchini, lakini msisite kukifungia chuo chochote kiwe cha umma au binafsi kama hakijakidhi vigezo vinavyotakiwa,” alisema Prof. Ndalichako.

Akifafanua alisema chuo ni mahali pa kupata elimu na maarifa si kupoteza muda na ndiyo sababu wanataka vyuo ambavyo wanafunzi wanaotoka pale wanakuwa na maarifa yatakayosaidia kufikia azima ya serikali ya uchumi wa viwanda.

Prof. Ndalichako alisema elimu siyo biashara na kama kuna mwekezaji mwenye dhana hiyo basi atafute biashara nyingine na si katika sekta hiyo.

Alisema anataka mwekezaji anayekuja kuwekeza katika elimu awe na dhamira ya dhati ya kutoa elimu na ustadi kwa watoto wa kitanzania na si kukusanya ada za wanafunzi na kufanya mambo binafsi tu.

Alisema nchi yoyote haiwezi kuendelea bila kuwa na wataalamu wa kutosha hivyo wanachukua hatua hizo ili kupata vyuo venye sifa ambavyo vitatoa watu wenye ujuzi watakaoendana na Sera ya Uchumi wa Viwanda.

 

Hata hivyo, alilitaka baraza hilo jipya kuendelea kubuni na kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato kwa lengo la kuboresha idara na kutatua changamoto zilizopo katika eneo wanalolisimamia.

Aidha, alipongeza baraza lililopita kwa kuvifanyia ukaguzi vyuo 464 na kati ya hivyo 20, vilifungiwa na vingine kuwekwa chini ya uangalizi.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Nacte, Dk. Adolf Rutayunga, alisema bado wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi na vitendea kazi jambo linasababisha kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

“Mpaka sasa tunawatumishi 71, lakini wanaotakiwa ni 201 hii ni asilimia 39 tu ya watumishi waliopo, changamoto hii inatukwamisha kutekeleza majukumu yetu," alisema.

Mwenyekiti wa baraza hilo, John Kondoro, alisema watashirikiana na wadau mbalimbali wa elimu kuhakikisha wanatatua changamoto zilizopo.

Habari Kubwa