Ndalichako aomba wawekezaji elimu

14Feb 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Ndalichako aomba wawekezaji elimu

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amewaomba wawekezaji na wadau katika sekta ya elimu nchini, kuwekeza katika Mkoa wa Dodoma kwa kuwa ndiko yaliko makao makuu ya nchi na kuna uhitaji mkubwa wa shule mkoa humo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa Shule ya Turkish Maarif iliyoko Boko, Profesa Ndalichako alisema serikali imejipanga kuboresha elimu nchini na hivyo kuwataka wawekezaji kujitokeza katika sekta ya elimu kutokana na upungufu wa shule uliopo.

“Kwa sasa makao makuu ya nchi yamehamia rasmi Dodoma, nawaomba wawekezaji na wadau wa elimu kuwekeza katika jiji letu la Dodoma kwa sababu bado kuna upungufu wa shule," aliomba.

Profesa Ndalichako alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau ambao watasaidia katika kuboresha sekta ya elimu nchini ili kutimiza azma yake ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora.

"Ndugu zetu kupitia taasisi yao ya Turkey Maarif Foundation, tunatambua sekta ya elimu ni muhimu sana katika taifa letu, hivyo tunawahamasisha kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine mfano Dodoma," alisema.

Waziri huyo alisema Uturuki imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania katika kuwekeza kwenye sekta ya elimu na kuwapongeza kwa hatua ya kujenga shule katika maeneo mbalimbali nchini, akizitolea mfano shule zao zilizoko katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar na Arusha na kuwakaribisha kujenga shule katika Mkoa wa Dodoma.

Alisema serikali imeipa kipaumbele sekta ya elimu kwa kutoa elimu bila malipo ikitenga zaidi Sh. bilioni 28 kila mwezi ili kuboresha sekta ya elimu nchini kama nyenzo umuhimu ya kufikia uchumi wa kati.

Akizungumzia shule za taasisi hiyo, Balozi wa Uturuki nchini, Ali Davutoglu, alisema wameamua kujenga shule hizo nchini kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Uturuki na amani iliyopo nchini.

"Shule hii tunayoizindua leo (jana), itahudumia wanafunzi 600, Turkish Maarif ni moja ya shule maarufu hapa Tanzania zenye takriban wanafunzi 1,900," alisema.

Habari Kubwa