Ndalichako atoa milioni 31 ujenzi bweni la wasichana Misungwi

11Nov 2019
Dotto Lameck
Mwanza
Nipashe
Ndalichako atoa milioni 31 ujenzi bweni la wasichana Misungwi

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ameahidi kutoa shilingi milioni 31 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bweni la wasichana katika shule ya sekondari Misungwi jijini Mwanza.

Ndalichako ametoa ahadi hiyo mara baada ya kufika shuleni hapo kukagua miundombinu ya shule hiyo na kuonesha kufurahishwa na uongozi wa shule kutumia fedha za visiting kwa kuweka akiba ya fedha ambazo zimewawezesha kuanza ujenzi wa bweni hilo.

“Nimefurahishwa sana na kitu mlichokifanya cha kuhifadhi fedha kidogokidogo kwa ajili ya kujenga bweni la watoto wa kike, hivyo basi mimi nikiwa waziri wa elimu lazima niunge mkono jambo hili ili kuhakikisha bweni hili linamalizika, kwahiyo nitatoa shilingi milioni 31 kwa ajili ya ujenzi” amesema Ndalichako.

Hata hivyo Ndalichako amesema kuwa pamoja na kutoa fedha hizo pia atahakikisha samani zinazohitajika katika bweni hilo zitanunuliwa.

Aidha, Ndalichako amewataka wanafunzi wa kike shuleni hapo kuzingatia masomo wawapo darasani na kutojiingiza katika mambo ambayo yanaweza kupelekea kuwakatishia masomo yao na kukatisha ndoto zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo Mwanani Asembandwa, amemshukuru Waziri wa Elimu kwa kutambua jitihada walizozifanya kwa ajili ya ujenzi wa bweni hilo la wasichana ambalo likikamilika litasaidia kutatua changamoto mbalimbali hasa kwa wanafunzi wa kike.

“tumefanikiwa kuwekeza fedha kidogokidogo hadi kufikia kupata shilingi milioni 44 ambazo zimetumika kuanza ujenzi wa bweni hili ambalo likikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 80” amesema Asembwanda.

Habari Kubwa