Ndama wa ajabu azua taharuki

25Feb 2020
Woinde Shizza
Arusha
Nipashe
Ndama wa ajabu azua taharuki

WAKAZI wa Kijiji cha Ngiresi Kata ya Sokoni 2 katika Halmashauri ya Arusha mkoani hapa, wameingiwa na hofu baada ya kuzaliwa kwa ng'ombe mwenye vichwa viwili, midomo miwili na macho matatu.

Hali hiyo imewashangaza wanachi hao kwa kile walichodai kuwa haijawahi kutokea wala hawajawahi kusikia imeotokea sehemu yoyote.

Aidha hali hiyo imewafanya wanakijiji kujitokeza kwa wingi kwenda kushuhudia ndama huyo alivyozaliwa, hali iliyomfanya mmiliki wa mnyama huyo kuzuia watu kwenda kumtazama.

Akizungumza na Nipashe, mmiliki wa ng’ombe huyo, Eliakimu Mungasi, alisema wakati anapewa taarifa ya ndama huyo alipata mshtuko kwa kuwa nijambo ambalo halijawahi kutokea katika maisha yake.

Mungasi alibainisha kuwa ng'ombe huyo alizaliwa Februari 3, mwaka huu na hadi sasa ana siku 23.

Alisema ng’ombe aliyemzaa ndama huyo ni uzao wake wa tano na kwamba awali alizaa salama na ng’ombe wenye afya lakini imemshangaza katika uzao wa safari hii.

“Watu wanasema mengi sana. Wengine wanasema ni uchawi wengine wanasema ni laana ya mababu. Lakini mimi sijali ninachokijua ni mpango wa Mungu na tutaendelea kumtunza hadi hapo atakapokufa,” alisema Mungasi.

Mke wa mmiliki wa ng'ombe huyo, Elizabeth Mungasi, alisema yeye ndiye alikuwapo wakati ndama huyo anazaliwa na alishitushwa kuona mnyama wa aina hiyo lakini alivumilia na kumpokea.

"Kwani ukizaa mtoto kilema unaweza kumuua? Sasa mimi kama mama nitamlea na nitakaa naye hadi pale ndama huyu atakapokufa. Tuliita daktari akaja akamwona akatuambia hana jinsi ya kutusaidia, kwa hiyo tukae naye hadi pale atakapokufa. Ndama huyu hawezi kula kitu tunachofanya ni kumkamulia maziwa na kumnyesha,"alisema.

Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Arusha, Charles Ngiroriti, alisema jambo kama hilo ni kawaida kutokea kwa wanyama.

Alibainisha kuwa katika utungaji wa kiumbe, inaweza kutokea chembe zikagawanyika kama vile zilitaka kutengeneza viumbe viwili lakini zikishindwa kugawanyika na kufika mwisho ndiyo anatokea kiumbe kama huyo.

Ngiroriti alisema hali hiyo haiusiani na imani za kishirikina, hivyo watu waache kuzusha maneno na waone ni hali ya kawaida kutokea.

Pia alisema mgawanyiko kama huo unaweza kufikia sehemu viungo vingine vifanye kazi na vingine kutofanya kazi, hivyo ndama huyo anaweza kukaa muda mrefu au mfupi.

Habari Kubwa