Ndege kutumika kudhibiti nzige, shule zafungwa siku 4

22Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Longido
Nipashe
Ndege kutumika kudhibiti nzige, shule zafungwa siku 4

WAZIRI wa Kilimo, Prof. Adolf Mkenda, jana alitembelea eneo la Longido ambalo limevamiwa na nzige na kutangaza kuwa kuanzia leo, ndege maalum itafanya kazi kupulizia viuatilifu kuua nzige hao.

Prof. Mkenda alisema wananchi wasiwe na hofu kwa kuwa nzige wote watadhibitiwa kupitia wataalamu wa Wizara ya Kilimo waliopo kwenye maeneo yote yenye dalili za uwapo wao.

"Kuanzia kesho (leo), ndege maalum itaanza kazi kupulizia sumu kuua nzige waliovamia maeneo ya Longido na Simanjiro," alisema Prof. Mkenda.

Waziri huyo alisema tayari wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kudhibiti Visumbufu (TPRI) wapo wilayani Longido na Simanjiro wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake, Dk. Efrem Njau.

Alitoa wito kwa wananchi kutookota wala kula nzige watakaokuwa wameuawa kwa viuatilifu kwenye maeneo yote ambapo ndege itapita kuua nzige.

Pia, aliagiza wataalamu na watendaji wa vijiji na kata kutoa taarifa kwa wananchi juu ya uwapo wa kazi ya kuua nzige, hivyo wasiwe na hofu.

"Wananchi wakiona nzige wameanguka chini, wamekufa, wasiwachukue au kula kwa kuwa wengi watakuwa wamekufa kwa sumu," Prof. Mkenda alionya.

Waziri huyo alisema serikali itahakikisha mazao ya wakulima na malisho ya mifugo hayaharibiwi na nzige, ndiyo maana ametembelea eneo hili la Longido na amebainisha mafanikio ya kuwadhibiti tangu walipoingia nchini Januari mwaka huu kwenye baadhi ya maeneo.

Prof. Mkenda alisema nzige wa jangwani wana athari kubwa katika uzalishaji wa mazao ya chakula  na malisho ya mifugo na kundi moja la nzige lina uwezo wa kuruka bila kutua kwa umbali wa kilometa 150 kwa siku.

"Nzige wana uwezo wa kula sawa na uzito wake kwa siku ambapo kundi moja la nzige linaweza kuwa na wastani wa nzige milioni 40 kwenye eneo la kilometa  moja za mraba," alifafanua Prof. Mkenda.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Jumaa Mhina, aliagiza shule zote za msingi na sekondari kwenye maeneo ambapo ndege itapuliza viuatilifu, kusitisha masomo kwa muda wa siku nne kuanzia kesho ili kudhidhibi watoto wasije wakapata madhara endapo watashika au kuchezea nzige watakaokufa.

Mbunge wa Longido, Dk. Steven Kiruswa, aliiomba serikali iharakishe kupulizia viuatilifu ili nzige wasisababishe madhara kwa mifugo na wakulima kwenye maeneo ya Longido.

"Leo (jana) ni siku ya tatu nzige wameingia Longido. Tunaomba jitihada za wataalamu wa TPRI kuwadhibiti ili wasilete madhara kwetu sisi wafugaji tunaotegemea nyasi kwa malisho," alisema.

Habari Kubwa