Ndege nyingine yaanguka

07Aug 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Ndege nyingine yaanguka

SIKU nne baada ya ajali ya ndege kutokea wilayani Sikonge mkoani Tabora, ajali nyingine ya usafiri huo wa anga ilitokea jana wilayani Mafia mkoani Pwani.

Mabaki ya ndege ya Shirika la Tropical Air yenye namba za usajili 5H-NOW, iliyopata ajali baada ya kuanguka wakati ikitaka kupaa katika kisiwa cha Mafia, mkoani Pwani jana.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ilieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ya Mafia ni ndege kukosa nguvu ya kupaa kwenye Uwanja wa Ndege wa Mafia.

Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TCAA, Hamza Johari, alisema ndege hiyo ya Shirika la Tropical Air yenye namba za usajili %H-NOW ilikuwa ikitokea Mafia kuelekea Dar es Salaam.

"Ilivyojaribu kupaa, ilishindwa kuinuka lakini baadaye iliinuka na ilivyokaribia mwisho wa eneo la kurukia (run way), iliinuka kidogo kama inapaa lakini haikwenda mbali ilirudi chini.

"Ilirudi chini na kuserereka kwenda kugonga uzio wa uwanja wa ndege, rubani alifungua mlango kwa haraka na abiria wote walitoka na baadaye ililipuka. Abiria wanne walipata majeraha madogo madogo na wanaendelea na matibabu Hospitali ya Mafia,” alisema.

Joari aliongeza kuwa TCAA itaendelea kutoa taarifa kwa umma baada ya wataalamu wake kufanya uchunguzi wao kwa ndege zote mbili.

“Tunafanya uchunguzi wa mara kwa mara, ndege zote zinazoruka angani ila bado ni vyombo vya moto na injini ni injini au mashine, huwezi kuwa na uhakika asilimia 100 kwa kuwa inaweza kuwa mpya na bado ikapata shida.

“Cha msingi ni kujua ilikuwa ni nini na nini kifanyike, lengo ni kuhakikisha kwamba ajali hazitokei na ndiyo maana tunaona inaweza kupita mwaka hazijatokea," alisema.

Jumapili iliyopita, majira ya asubuhi, katika Kijiji cha Mahompa, Kata ya Igigwa wilayani Sikonge, ilitokea ajali ya ndege yenye namba za usajili ZU-TAF aina ya Sling Aircraft na kusababisha vifo vya abiria, rubani na msaidizi wake.

Habari Kubwa