Ndege za 1920, 1930 kutangaza utalii nchini

24Nov 2016
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Ndege za 1920, 1930 kutangaza utalii nchini

JUMLA ya ndege 22 za zamani ambazo zilizotengenezwa kati ya miaka ya 1920 na 1930 zinatarajia kuwasili nchini, Novemba 28 hadi Desemba 2, 2016, kushiriki kwa ajili ya mashindano ya anga.

Meneja Mkuu wa kampuni ya Puma Energy, Philippe Corsaletti

Lengo la mashindano hayo ni kutangaza utalii wa Tanzania kimataifa.

Meneja Mkuu wa kampuni ya Puma Energy inayofadhili ujio wa ndege hizo, Philippe Corsaletti, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa ndege hizo aina ya Vintage Air Rally zitatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) zikitokea uwanja wa ndege wa Wilson jijini Nairobi, Kenya.

Alisema ndege hizo zitakazokuwa na marubani takribani 50, watakapofika nchini watakwenda kutembelea mbuga za wanyama na Puma itasaidia katika kuweka utalii wa Tanzania katika mtazamo wa kimataifa.

Corsaletti alisema ndege hizo zinafuatiliwa na maelfu ya watu kwa kuwa zimeshazunguka nchi kadhaa duniani.

“Kampuni ya Puma Energy Tanzania tumejiandaa kupokea ugeni huu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma zote za kujaza mafuta ili kuhakikisha urukaji ulio salama,” alisema na kuingeza:

“Tumejiandaa kupokea na kuhudumia msafara mzima katika kiwango cha juu cha ubora na ufanisi. Uwapo wa bohari zetu za mafuta ya ndege katika maeneo mbalimbali nchini unafanya iwe rahisi kuhudumia ndege hizo ambako zitapita.”

Alitaja mikoa ambayo ndege hizo zitatua kuwa ni Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Zanzibar, Dodoma, na Songwe kabla ya kuelekea Zambia na kupokelewa na kuhudumiwa na wenzeo wa Puma Zambia.

Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo la kihistoria wakati ndege hizo zitakapokuwa zikipita katika maeneo yao.

Habari Kubwa