Ndejembi aitaka TAKUKURU kuchunguza ujenzi karakana ya walemavu

04Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Katavi
Nipashe
Ndejembi aitaka TAKUKURU kuchunguza ujenzi karakana ya walemavu

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi, amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi kufanya uchunguzi wa ujenzi wa mradi wa jengo la karakana ya watu wenye mahitaji maalumu mkoani Katavi-

-ambalo liliwezeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao haujakamilika mpaka sasa.

Akizungumza na viongozi wa Chama cha Walemavu mkoani humo ambao ndio waasisi wa mradi huo, Ndejembi amesema TASAF ilitoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha wenye ulemavu mkoani Katavi kujenga karakana hiyo ili waweze kufanya shughuli zao kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.

Amesema watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii, na licha ya kuwa na ulemavu wameonyesha dhamira ya kujishughulisha na kutoa mchango kwa maendeleo ya taifa, hivyo wanapaswa kuungwa mkono na Serikali pamoja na jamii kwa ujumla.

Ndejembi ameongeza kuwa, chama hicho cha walemavu kilikuja na wazo la kuanzisha mradi huo ili wajishughulishe na ushonaji na kuwa na ofisi ya kikundi ambayo itaratibu ushiriki wao katika uzalishaji kwa manufaa ya Taifa, hivyo atakaa na uongozi wa TASAF ili kuangalia namna ya kuwezesha ukamilishaji wa ujenzi huo baada ya uchuguzi wa TAKUKURU kukamilika.

Ndejembi amesisitiza umuhimu wa TAKUKURU kukamilisha uchunguzi kabla ya kuendelea na ujenzi wa mradi huo, lengo likiwa ni kujiridhisha na matumizi ya fedha zilizotolewa awali pamoja na kulinda hadhi ya Mwenge wa Uhuru ambao Kiongozi wake aliweka jiwe la msingi tarehe 20 Septemba, 2012.

Habari Kubwa