Ndikilo ahamasisha lishe bora Pwani

20Jul 2020
Julieth Mkireri
Kibaha
Nipashe
Ndikilo ahamasisha lishe bora Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, amewataka wakuu wa wilaya za mkoa huo kusimamia kikamilifu suala la lishe bora katika wilaya zao.

Ndikilo alitoa rai hiyo wakati akifungua kikao cha pili cha tathmini ya mkataba wa lishe kwa kipindi cha Januari-Juni, 2020, kilichofanyika Julai 16, mjini Kibaha.

Aliwataka viongozi hao wa wilaya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu lishe bora na itakayoambatana na kuhamasiha watoto kupewa chakula wakiwa shuleni.

“Ndugu wajumbe tumeona tatizo la udumavu kitaifa ni asilimia 31 na sisi katika mkoa wetu tuna asilimia 23 kutokana na hali hii wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na wataalamu wa afya tunatakiwa kusisitiza lishe bora kila mmoja katika eneo lake," alisema Ndikilo.

Alisema baada ya agizo hilo anatarajia kupata matokeo chanya kwa kila mmoja kusimamia katika eneo lake na kuhakikisha asilimia hiyo inapungua pamoja na kuondoa idadi ya watoto wenye udumavu inapungua.

Alitoa wito kwa wazazi wenye watoto shuleni kuwachangia chakula ili waweze kuepuka tatizo la udumavu kwa kukosa chakula.

Aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kwa kuvuka malengo ya kiwango kilichowekwa cha viashiria vya mkataba wa lishe na kuzitaka halmashauri nyingine za mkoa huo kuiga mfano wa halmashauri hiyo.

Habari Kubwa