Ndugai anusa harufu ya rushwa upimaji magari kwenye mizani

27Jan 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe Jumapili
Ndugai anusa harufu ya rushwa upimaji magari kwenye mizani

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ameshangazwa magari kupita katika vituo vingi vya mizani na kupimwa huku akisema kuna mazingira ya rushwa katika kufanya hivyo.

SPIKA WA BUNGE JOB NDUGAI

Ndugai alisema hayo jana wakati akifungua semina ya wabunge juu ya changamoto na mafanikio ya sheria ya vipimo ambayo wabunge walielimishwa jinsi ya kupambana na rushwa katika vipimo.

 

Alisema magari ya mizigo yakiwamo yanayosafirisha mafuta, licha ya kupita katika mizani mbalimbali, bado yanazuiwa baadhi ya sehemu kwa sababu ya kutakiwa kupimwa tena.

 

Alisema hatua hiyo imekuwa ikiwakera wananchi kwa kuwa hawaelewi tatizo mpaka kuwapo kwa vipimo kila sehemu na kufanya msururu wa magari kuwa mkubwa barabarani.

 

“Kama ni magari ya mizigo inawezekana wakaongeza njiani lakini kama wale wanaosafirisha mafuta kweli jamani tuliangalie na hilo nalo,"alisema.

 

Ndugai alisema hali hiyo ni chimbuko la rushwa kwa kuwa kama mfanyabiashara anayesafirisha mafuta ameshapima vituo vyote hakuna sababu ya kumzuia kwani uwezekano wa kuongeza ujazo wa mafuta njiani ni mdogo.

 

Pia alisema bado kuna tatizo katika vipimo sahihi wakati wa ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima licha ya kuwapo kwa Sheria ya Vipimo ya mwaka 1982.

 

Wabunge  walioshiriki semina hiyo ni wanachama wa hiari wa Chama cha Wabunge cha Kupambana na Rushwa (APNAC) ambao hutoa michango juu ya kupambana na vitendo hivyo.

 

Ndugai alisema wakulima wamekuwa wakinyonywa na baadhi ya wafanyabiasha kwa kutumia vipimo ambavyo si sahihi ikiwamo ufungashaji wa mazao kwa njia ya lumbesa.

 

“Rasilimali nyingi zimekuwa zikipotea kutokana na ufungashaji kwa njia ya lumbesa na njia nyinginezo ambazo si rasmi. Tufikie wakati tuwe na sheria kali zaidi kwani wakulima wetu wamenyonywa na kupunjwa vya kutosha,” alisema.

 

Awali akitoa taarifa ya  kwa wabunge wanachama wa APNAC,  Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Mtuka, alisema madhumuni yao ni kupambana na rushwa.

 

Alisema wabunge waliokuwapo kipindi hicho waliona kuna umuhimu wa kuanzisha kikundi cha wabunge ambao watapambana na rushwa nchini.

 

“APNAC mwaka 2007 ilishiriki kuandaa sheria Na. 11 ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru). Sheria hiyo ilikuwa na vifungu vinne tu lakini sasa vipo 24” alisema.

 

Hata hivyo alisema sheria hiyo bado ina changamoto hivyo inahitaji kufanyiwa marekebisho zaidi.

 

“Tumetoa marekebisho mengi juu ya Sheria ya Takukuru na mengi yamesaidia nchi yetu lakini bado tunaona ipo haja ya kuendelea kutoa mawazo yetu,"alisema.

 

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, alisema bado kuna changamoto kubwa katika suala la vipimo nchini kwa kuwa kumekuwa na udanganyifu mkubwa kwa wafanyabiashara na madalaliwakati wa kufanya ununuzi toka kwa wakulima.

 

“Vipimo kama vya lumbesa, madebe na hata vikopo bado vimekuwa vikitumika katika sehemu nyingi nchini ingawa tunavikataa,”alisema.

 

Kakunda alisema wizara yake imeweza kujenga vituo vya masoko katika mipaka ilikuwawezesha wakulima kuuza kwa faida.

 

 

Habari Kubwa