Ndugai apigiwa debe u-Spika

07Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Ndugai apigiwa debe u-Spika

RAIS John Magufuli amempigia debe Spika wa Bunge, Job Ndugai, akisema atashangaa kama Bunge lijalo hawatamchagua kushika wadhifa huo kutokana na mambo makubwa aliyofanya ikiwamo kutungwa kwa sheria bora ya madini.

Magufuli alisema hayo jana jijini hapa alipokuwa akizungumza na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Makao Makuu ya chama hicho, baada ya kuchukua fomu ya kuomba kugombea urais katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) kupitia CCM.

“Namshukuru sana Spika, nitashangaa sana bunge linalokuja wakaacha kukuchagua wewe. Watasema nakupigia kampeni, nina haki kwani uliunda Tume ya Madini kwenda kuchunguza na ripoti akaileta na tukabadilisha sheria,” alisema.

Sheria hiyo, alisema ni sheria bora nchini kwa kuwa madini sasa yanapatikana na fedha zinazotokana na rasilimali hiyo zinapelekwa kwenye miradi ya maendeleo.

“Tunaijenga nchi yetu ndiyo maana leo mnaona hata Mmasai Laizer anapata madini ya kilo 10. Zamani mbona yalikuwa hayaonekani? Hii ni kwa sababu tumejenga ukuta ndiyo maana ndugu zangu wana CCM katika kufikiria haya kwamba tumehangaika hivi, tukiondoka wale wenye rangi nyingine ambayo si ya kijani watakuja kuyafanya haya.

“Walikuwa wanashirikiana na mabeberu kutuibia madini yetu leo kweli wataweza kulinda madini yetu? Ndiyo maana nimesema potelea mbali nagombea miaka mingine mitano. Tanzania hii ni taifa tajiri, lakini tulizoeshwa kuambiwa maskini ndiyo maana tumeingia kwenye uchumi wa kati na tumeingia kwa sababu mali yetu ilikuwa inaibwa sasa tumeidhibiti vizuri.

Naye Spika Ndugai alimhakikishia Rais Magufuli kuwa atapata kura nyingi Dodoma na nchi nzima kutokana na mambo aliyoyafanya.
“Dodoma hatuna cha kukulipa isipokuwa kukupa kura. Wana CCM tujipange twende kaya kwa kaya. Wale wenzetu hawana la kusema, wengine wagomvi tu,” alisema.

Makamu wa Rais na Mgombea Mwenza, Samia Suluhu Hassan, alisema vifo vya wanawake na watoto vilivyokuwa vinaliliwa vimepungua kwa kiwango kikubwa.

“Tulikuwa tunalia na vifo vya wanawake vimepungua kwa kiasi kikubwa, tatizo la maji kwa asilimia 74 limepungua. Tulikuwa tunalia tatizo la ada kwa watoto wetu umetupokea huo mzigo tunashukuru sana, umetung’arisha katika majumba yetu mapya hadi vijijini kwenye matembe kwa kutuletea umeme,” alisema.

Aliahidi kwa niaba ya wanawake na Watanzania watafanya kazi bega kwa bega naye ili kulinda heshima aliyowapa.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ali, alisema mitambo ya ushindi kwa chama hicho imewashwa rasmi jana huku akitaja majukumu ya jumuiya za chama hicho katika kuhakikisha ushindi wa kishindo unapatikana.

“Kuhamasisha wananchi kupiga kura nyumba kwa nyumba, kitanda kwa kitanda, mtaa kwa mtaa, shuka kwa shuka na kulinda kura jukumu hili tumelikabidhi kwa Jumuiya ya Vijana wa CCM(UVCCM),” alisema.

Habari Kubwa