Ndugai ataja hatua nne za kuchukua kukuza kilimo

17Apr 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Ndugai ataja hatua nne za kuchukua kukuza kilimo

SPIKA wa Bunge Job Ndugai ametaja hatua nne za kuchukua kwa ajili ya maendeleo ya biashara zitokanazo na mazao ya kilimo na viwanda vitokanavyo na usindikaji mazao hayo.

SPIKA wa Bunge Job Ndugai.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo alipokuwa akifungua Mhadhara wa umma kuhusu mwelekeo wa upatikanaji wa chakula, kukuza mnyororo wa thamani wa bidhaa zitokanazo na kilimo duniani ambao umeendeshwa na Chuo cha Usimamizi wa Fedha(IFM), ukumbi wa Pius Msekwa.

Ametaja hatua hizo kuwa ni serikali lazima iendelee kuweka mazingira mazuri ya sera ambazo zitawafanya wafanyabiashara wadogo na wa kati na viwanda vinavyosindika mazao ya kilimo kukua na kustawi.

“Pili, Wazalishaji wadogo wanahitaji msaada kuwawezesha kushindana katika soko la ndani, kikanda na kimataifa, kwa mfano mafunzo yanaweza kusaidia kuboresha stadi zao za usimamizi mzuri wa shughuli zao.Hili IFM mnaweza kusaidia kutoa elimu na stadi za biashara katika kilimo,”amesema.

Nyingine ni upatikanaji dhaifu wa huduma za fedha kwa muda mrefu zimedumaza maendeleo vijijini nchini Tanzania.

Ndugai ametaja hatua ya nne ni uwekezaji katika utafiti wa kilimo ni muhimu ili kuibua teknolojia mpya katika kilimo ambazo zinaweza kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Hata hivyo amesema rasilimali fedha za kutosha zinapaswa kuelekezwa katika tafiti za kilimo ili kuhakikisha kwamba wakulima wadogo wanaweza kukabiliana na mabadiliko hayo kwa kutumia mbegu bora.

Habari Kubwa