Ndugulile ataka kasi matumizi Tehama SADC

28Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ndugulile ataka kasi matumizi Tehama SADC

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile, amezitaka Mashirika na makampuni ya mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika kuhakikisha zinaongeza kasi ya matumizi ya mawasiliano na TEHAMA katika kuleta maendeleo ya Uchumi.

Dk. Ndugulile ameyasema hayo baada ya kufungua Mkutano wa 41 wa Mashirika na makampuni ya mawasiliano katika nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika (SADC) unaojulikana kama Southern Africa Telecommunications Association (SATA) ambao umefanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma na nchi 23 zimeshiriki kikao hicho.

Dk. Ndugulile amesema kuwa nchi wanachama katika SADC watumie fursa mbalimbali zinazopatikana kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano hasa matumizi ya intaneti kuwa yanawezesha kufanyika kwa shughuli za biashara, uchumi na maendeleo kwa ujumla.

“Kama tukiboresha mawasiliano katika nchi zetu za SADC, hii itasaidia kuongeza na kukuza biashara katika nchi zetu, baada ya mimi kwenda benki kulipia niweze kutumia simu yangu kuweza kununua bidhaa kutoka nchi wananchama,” amesema.

Dk. Ndugulile amesema kuwa anatamani kuona gharama za mawasiliano baina ya nchi hizo za Afrika zinapungua kwa kutengeneza mfumo madhubuti wa kuwa na mawasiliano ya ndani ya Afrika (Regional Hub) badala ya kusafirishwa kwenda nchi za ulaya na marekani ndipo yarudi na kumfikia mlengwa.

“Serikali imewezesha kuwa na mawasiliano ya ndani kama nchi hivyo kushusha gharama za huduma za mawasiliano ambapo miongoni mwa zinazofanya vizuri sana kwenye huduma za kifedha kupitia makampuni ya simu ni Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zinazoongoza katika bara la Afrika,” amezungumza.

Habari Kubwa