NEC yawapiga msasa wasimamizi uchaguzi

01Aug 2020
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
NEC yawapiga msasa wasimamizi uchaguzi

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi ngazi za majimbo, katika Mkoa wa Shinyanga na Simiyu, ili kufanikisha uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu, ufanyike kwa haki na huru.

Wasimamizi wa uchaguzi kutoka Shinyanga na Simiyu wakila kiapo.

Akifungua mafunzo hayo leo mjini Shinyanga Kamishina wa NEC, Balozi Omari Mapuli, amesema NEC inaendesha mafunzo kwa wasimamizi hao wa uchaguzi pamoja na wasaidizi wao, wakiwamo na maofisa ugavi, ili kuwajengea uwezo namna ya kusimamia zoezi zima la uchaguzi mkuu.

Amesema wameendesha mafunzo hayo ili kufanikisha zoezi zima la uchaguzi mkuu linafanyika kwa ufanisi na kuondoa malalamiko kwa vyama vya siasa, na umalizike kwa amani bila ya kutokea vurugu zozote zile, kwa kuzingatia katiba ya nchi, sheria za uchaguzi, maadili na kanuni zake.

“Tume ya taifa ya uchaguzi tunatoa mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo na wasaidizi wao kutoka Shinyanga na Simiyu, lengo ni kuhakikisha uchaguzi mkuu ambao utafanyika Oktoba 28 mwaka huu, unafanyika kwa haki na huru na kumalizika kwa amani,” amesema Mapuli na kuongeza kuwa;

Kamishina wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Balozi Omari Mapuli akifungua mafunzo ya wasimamizi wa uchaguzi Mkoa wa Shinyanga na Simiyu.

“Mnatakiwa kutambua kuwa mmeaminiwa na tume, na kuteuliwa kufanya zoezi hili la kusimamia uchaguzi, jambo la muhimu ni kujiamini, kujitambua, pamoja na kuongozwa na katiba ya nchi, sheria ya uchaguzi, maadili na kanuni zake wakati wa kutekeleza majukumu yenu ili kuhakikisha uchaguzi una malizika salama,” ameongeza.

Kwa upande wake Mratibu wa Uchaguzi mkoani Shinyanga Fabiani Kamoga, amesema mafunzo hayo yanatija kubwa kwa wasimamizi hao wa uchaguzi ngazi ya majimbo, ambapo pia watayashusha ngazi ya Kata, ili uchaguzi mkuu ufanyike kwa haki na huru, bila kutokea malalamiko yoyote yale kwa vyama vya kisiasa.

Habari Kubwa